NA.MATUKIO DAIMA ,SAME.
TAASISI ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imetoa elimu kuhusu tahadhari za majanga ya asili, masuala ya jiolojia na El Nino kwa wakazi wa kijiji cha Mamba Miamba, Jimbo la Same Mashariki, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro.
Elimu hiyo ilitolewa katika kikao kilichofanyika leo kilichowakutanisha viongozi wa Serikali ya Kijiji, Mtendaji wa Kijiji pamoja na wananchi, ambapo walijadili hatua mbalimbali za kuchukua ili kupunguza athari za majanga ya asili katika eneo hilo.

Kikao hicho kilifanyika kufuatia ombi la Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, alilolitoa Septemba 28 mwaka huu mara baada ya semina iliyowakutanisha maafisa tarafa, madiwani na watendaji wa kata.
Katika semina hiyo, pamoja na kutembelea baadhi ya maeneo hatarishi upande wa tambarare, mbunge huyo aliwaomba wataalamu kufika katika maeneo ya milimani kwa ajili ya kutoa elimu na ushauri wa kitaalamu.
Katika kikao hicho, wananchi walikubaliana kusitisha mara moja shughuli za kilimo katika eneo lililowahi kuathiriwa na maporomoko ya udongo mwaka 2009. Badala yake, walikubaliana kupanda miti katika eneo hilo ili kusaidia kurejesha uimara wa udongo na kupunguza mmomonyoko.
Aidha, wananchi waliiomba Serikali kuchukua hatua za kudhibiti athari za radi katika eneo hilo, ikiwemo kuweka mifumo au vifaa maalumu vya kinga dhidi ya radi, kutokana na eneo hilo kuwa na historia ya kukumbwa na matukio ya radi mara kwa mara.
Wataalamu wa GST pia waliwasisitiza wananchi kuendelea kufuatilia taarifa na tahadhari zinazotolewa na mamlaka husika kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na majanga ya asili, pamoja na kuchukua hatua mapema wanapoona dalili zinazoweza kuhatarisha usalama wa watu na mali.
GST imeendelea kutoa elimu kwa jamii katika maeneo mbalimbali nchini kuhusu masuala ya jiolojia, majanga ya asili na namna ya kuchukua tahadhari, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa wananchi na kupunguza athari za majanga yanayoweza kujitokeza.

0 Comments