Header Ads Widget

WAFANYABIASHARA WA LIBRARY ZA VIDEO IRINGA WATISHIA KUTOFANYA KAZI NA UMOJA MOVIES


NA MATUKIO DAIMA MEDIA, IRINGA

UMOJA wa wafanyabiashara wa filamu maarufu kama Library za Video mkoani Iringa umeazimia kusitisha kwa muda kufanya kazi na kampuni ya Umoja Movies, ili kutoa nafasi kwa viongozi na wawakilishi wa wadau kukutana na kampuni hiyo kujadili changamoto zinazodaiwa kujitokeza katika mfumo mpya wa usambazaji wa kazi za filamu.

Akizungumza na wafanyabiashara hao katika ukumbi wa Manispaa ya Iringa, Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Library Mkoa wa Iringa, Joshua Sanga  amesema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadau kuhusu mfumo mpya uliowekwa na kampuni hiyo, hivyo kuna umuhimu wa pande zote kukutana na kutafuta suluhisho.

Sanga alisema moja ya hoja zinazohitaji ufafanuzi ni suala la usalama wa mfumo huo, hususan namna unavyolinda kazi pamoja na taarifa zilizohifadhiwa katika kompyuta za watumiaji.

Kwa mujibu wa Sanga  wafanyabiashara wanahitaji kupewa maelezo ya kutosha kuhusu mfumo huo na namna unavyofanya kazi kabla ya kuanza kuutumia kwa kiwango kikubwa.


Alisema ni muhimu kampuni kuwashirikisha wadau wanaotumia mfumo moja kwa moja kabla ya kuanzisha mabadiliko makubwa, ili kupata maoni yao na kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza kabla ya utekelezaji kamili.

Mwenyekiti huyo amesema wafanyabiashara wa filamu na kampuni wanapaswa kukaa pamoja na kujadiliana ili kubaini namna mfumo huo utakavyoweza kuwa na manufaa kwa pande zote.

“Umoja Movies inafanya biashara kwa lengo la kupata mapato, huku wadau nao wakitegemea kazi hizo kama chanzo cha kipato, hivyo ni muhimu kuwepo kwa usawa wa maslahi,” amesema.

Ameongeza kuwa wamependekeza utekelezaji wa mfumo huo usitishwe kwa muda ili kutoa nafasi kwa viongozi na wawakilishi wa wafanyabiashara kufanya mazungumzo na kampuni.


“Kuanzia sasa napendekeza kampuni kusitisha utekelezaji wa mfumo huo kwa muda ili kutoa nafasi kwa viongozi na wawakilishi wa wadau kukutana na kampuni na kujadili kwa kina changamoto zilizopo pamoja na namna bora ya kuendesha mfumo huo,” amesema.

Sanga alisema iwapo kampuni itaendelea na mfumo huo bila kufikiwa kwa makubaliano, umoja huo utaangalia njia nyingine zitakazowawezesha wanachama wake kuendelea kufanya kazi na kujipatia kipato.


Amefafanua kuwa hatua hiyo hailengi kuvunja ushirikiano uliopo, bali inalenga kuhakikisha maslahi ya wafanyabiashara na wadau wengine katika sekta hiyo yanazingatiwa.

Amesisitiza kuwa umoja huo una malengo ya kuwaunganisha wafanyabiashara wa filamu pamoja na kuibua fursa kwa vijana wenye vipaji na wanaotegemea biashara hiyo kama chanzo cha ajira na kipato.

Amesema Mkoa wa Iringa una vijana wengi wenye uwezo na vipaji ambao wanahitaji mazingira rafiki ya kuendeleza shughuli zao na kujipatia kipato.


“Nawaomba wanachama tuendelee kushikamana na kuwa na sauti moja katika masuala yanayotuhusu, kwa sababu umoja ndio msingi wa kupata suluhisho la changamoto zetu. Kupitia ushirikiano huo tunaweza kujenga mazingira bora ya kufanya biashara ya filamu na kuhakikisha sekta hiyo inanufaisha pande zote,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu wa Wafanyabiashara wa Library za Video, Erick Mushi, amesema baadhi ya watumiaji wamedai kukumbana na changamoto za kiufundi katika matumizi ya mfumo huo, ikiwemo kutofanya kazi kwa ufanisi katika baadhi ya kompyuta zinazotumia matoleo tofauti ya mfumo wa Windows.


Mushi amesema changamoto hizo zimejitokeza baada ya mfumo kuanza kutumika, hivyo wameomba kupewa muda wa kutosha kuujifunza, kuufanyia majaribio na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali kabla ya utekelezaji wake kwa kiwango kikubwa.TAZAMA FULL VIDEO BOFYA HAPA

Amesema wanaamini mazungumzo kati ya kampuni na wafanyabiashara yanaweza kusaidia kupata suluhisho litakalolinda maslahi ya pande zote na kuwezesha biashara ya filamu kuendelea katika mazingira mazuri.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI