Header Ads Widget

TGNP, WADAU WAIMARISHA VITA DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA MOROGORO

 


Na Deogratius Temba,Matukio Daima Media , Morogoro

Wadau wa ulinzi na kupinga Ukatili wa Kijinsia wameahidi kuimarisha ushirikiano na mifumo ya rufaa ili kuhakikisha waathirika wanapata huduma kwa wakati, huku jamii ikishirikishwa zaidi katika kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukatili.

Ahadi hiyo imetolewa katika mafunzo yaliyoandaliwa na Tanzania Gender Networking Programme (TGNP) kupitia Mradi wa Wanawake wa Vijijini katika Kuleta Mabadiliko (WRCC), unaotekelezwa katika Halmashauri za Gairo na Morogoro.



Mradi huo pia unalenga kuboresha maisha ya wanawake, wanawake vijana na watu wenye ulemavu kwa kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uzalishaji na uchumi wa kaya kupitia kilimo ikolojia. 

Mafunzo hayo yamewakutanisha Maafisa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji, Kamati za MTAKUWWA pamoja na washiriki kutoka Vituo vya Taarifa na Maarifa vya Kata za Rubeho, Gairo DC, na Tomondo, Morogoro DC.

Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, Polisi Kata wa Tomondo, Mkaguzi wa Polisi Elias Mwinyi, alisema elimu aliyopata imeongeza maarifa na kukuza utendaji wake, sambamba na kupanua wigo wa ushirikiano na wadau katika jamii, wakiwemo Vituo vya Taarifa na Maarifa na Kamati za MTAKUWWA.



 “Tumepata elimu nzuri, tutakuwa mabalozi wa kuendeleza elimu hii, lakini kusimamia kikamilifu miongozo ya kuzuia na kutokomeza vitendo vya Ukatili wa Kijinsia.Tutajitahidi kuwa vinara wa kupinga Ukatili,” alisema. Aliongeza kuwa kazi ya kupambana na Ukatili wa Kijinsia inahitaji kujitolea na uzito wa kipekee kwa kuwa inalenga kulinda usalama na ustawi wa jamii.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Kata ya Tomondo, Koronely Mkombo, alisema mafunzo hayo ni mwanzo mpya wa kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya Ukatili wa Kijinsia, hasa kwa kuunganisha nguvu za wadau wanaopatikana ndani ya kata.


 Naye Afisa Maendeleo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Perpetua Nguya, alisisitiza umuhimu wa washiriki kutumia maarifa waliyoyapata kuboresha utendaji wao wa kila siku na kuimarisha ushirikiano katika ngazi ya jamii. 



Kwa mtazamo mpana, juhudi hizo zinaendana na malengo ya WRCC ya kujenga jamii yenye uwezo wa kuwawezesha wanawake, wanawake vijana na watu wenye ulemavu kushiriki katika maamuzi, uzalishaji na maendeleo, huku ikolojia na usalama wa jamii vikipewa nafasi katika kujenga maisha yenye ustahimilivu.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka TGNP, Deogratius Koyanga, alisema mapambano dhidi ya Ukatili wa Kijinsia hayawezi kufanikiwa kwa taasisi moja kufanya kazi peke yake, bali yanahitaji mfumo unaowaunganisha jamii, serikali, Polisi, afya, Ustawi wa Jamii, msaada wa kisheria na wadau wengine. 


Katika mafunzo hayo, washiriki walitumia mbinu shirikishi kuchora ramani ya safari ya mwathirika wa ukatili, kubaini hatua anazoweza kupitia kutoka wakati wa tukio hadi kupata huduma, pamoja na maeneo ambayo mfumo wa rufaa unafanya vizuri, yanayohitaji kuboreshwa au ambayo bado yana mapengo. 

“Lengo si kulaumiana, bali kuufanya mfumo ufanye kazi vizuri zaidi kwa kuanzia kwenye tatizo, kutambua chanzo chake, kubuni suluhisho na kukubaliana nani afanye nini, lini na kwa kipimo gani cha mafanikio,” alisisitiza Koyanga.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI