Na: Mwandishi Wetu, Zanzibar
ZANZIBAR - Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga amepongeza tamasha la FuToPiA Zanzibar kwa kuanzisha jukwaa la ubunifu linalowezesha wadau mbalimbali kutoa mawazo juu ya ukuaji wa uchumi, masuala ya kidijitali na masoko.
Soraga amesema hayo katika jukwaa maalum la ubunifu wakati wa msimu wa pili wa tamasha la Muziki, Utamaduni na Ubunifu la FuToPiA Zanzibar, lililofanyika Fumba Town, Unguja tarehe 8 na 9 Agosti, 2026.
Katika jukwaa hilo, Soraga ameshiriki majadiliano maalum kuelezea mikakati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, SMZ katika safari ya mageuzi ya kidijitali katika visiwa vya Zanzibar.
Amesema Zanzibar kwa sasa inapitia vipindi tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma kama kisiwa. Uchumi unakua kwa haraka na kila pembe kuna fursa za kiuchumi zinazojitokeza ikiwemo miradi ya maendeleo.
![]() |
| Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga |
Aidha, amesema wao kama viongozi wa Serikali wanapongeza wadau kuja na majukwaa ya ubunifu kwani yanaisaidia Serikali kufikia malengo yake kwa ushirikiano na wadau.
"Kupitia majukwaa kama haya ya tamasha la FuToPiA Zanzibar, tunapata fursa ya kuelezea harakati na vipaombele vya Serikali tunavyotarajia kuvifanyia kazi kwa wananchi," amesema Soraga.
Ameeleza kuwa Serikali ya SMZ ina mipango ya kuweka miundombinu ya TEHAMA na mawasiliano ili wananchi wote waweze kuunganishwa na mtandao. Hii ni pamoja na kuweka mtandao wa wazi 'Public Wi-Fi' Zanzibar nzima.
Pia amesema Serikali imejipanga kuboresha mifumo ya ulinzi ili kulinda udukuzi wa taarifa katika mitandao ya simu, kibenki na huduma nyingine ili zibaki katika hali ya usalama.
Kuhusu ubunifu hususani kwa vijana wa Zanzibar, Soraga amesema Serikali imeweka nguvu kubwa ya kuunda mazingira bora na rafiki kwa vijana kuonesha vipaji vyao ikiwemo ubunifu wa mifumo na huduma za kidijitali. Amesema vijana watapewa nyenzo na maarifa ili waweze kutengeneza mifumo na kutoa masuluhisho mbalimbali.
Ameongeza kuwa Serikali ipo katika mpango wa kuboresha miundombinu ya msingi ya TEHAMA ikiwemo njia za kimataifa za mtandao wa intaneti 'International Gateway' na kuwa na kituo cha data 'Data Center' cha kuhifadhi taarifa. Amesema Serikali imekusudia kuwekeza zaidi ya dola za Marekani milioni 100 mpaka kukamilika kwa mradi huo.
Katika kuhakikisha huduma zinapatikana kwa urahisi, amesema watafanya kazi ya kuunganisha mifumo ndani ya Serikali hasa ya utoaji wa huduma ili kumsaidia mwananchi.
Kuhusu matumizi ya fedha taslimu, amesema dunia ya sasa inatakiwa kuachana na matumizi ya fedha taslimu na kuelekea kwenye matumizi ya mifumo ya fedha kupitia mitandao.
"Nichukue fursa hii kumpongeza na kumshukuru Rais wetu Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa utashi wake mkubwa na muelekeo alioutoa wa kuona Zanzibar ifikapo 2030 suala zima la matumizi ya fedha taslimu liwe historia na kwamba wananchi wote waweze kulipia huduma zao kwa njia ya mtandao, kibenki na kwenye simu," amesema Soraga.
Tamasha la FuToPiA Zanzibar linaandaliwa na Busara Promotions na linajumuisha muziki, sanaa, ubunifu, masoko na michezo.
Wasanii na ma-DJ mbalimbali walioshiriki ni pamoja na DJ Joozey, DJ Zoro, Baba Kash, Sauti Marley, Ruth Mlawa, DJ LAG kutoka Afrika Kusini, Vania Ice, Hammer Q na wengineo.









0 Comments