Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Agosti 21, 2026 imemruhusu mtoto aliyefanyiwa upasuaji wa kwanza wa kutenganishwa na pacha aliyeungana aina ya parasitic conjoined twins, baada ya kuendelea vizuri kwa siku 10 tangu kufanyika kwa upasuaji huo wa kihistoria.
Akizungumza baada ya kuruhusiwa kutoka Hospitalini hapo, Bi. Glory Nyambeke, mama wa mtoto huyo, ameishukuru timu ya madaktari bingwa kwa kuokoa maisha ya mwanaye, akisema mafanikio ya matibabu hayo yameirejeshea familia yake matumaini na furaha baada ya kipindi kigumu cha hofu na mashaka.
Kwa upande wake Bingwa wa Upasuaji wa Watoto wa MNH, Dkt. Victor Ngotta, amesema kuruhusiwa kwa mtoto ni jambo linalowapa furaha kubwa wataalam walioshiriki upasuaji huo, kwani ni matokeo ya kazi ya pamoja, maandalizi ya kina na ufuatiliaji wa karibu uliofanyika tangu siku ya upasuaji.
Amesema mafanikio hayo yanaonyesha uwezo wa madaktari wazawa kufanya upasuaji tata na wa aina ya kipekee nchini, huku yakiendelea kuimarisha nafasi ya Muhimbili kama kituo kinachoongoza katika huduma za ubingwa na ubingwa bobezi.






0 Comments