Header Ads Widget

NCAA YAPITISHA WANAFUNZI 33 WATAKAOJIUNGA NA VYUO VYA KATI SEPTEMBA ,2026 KUPITIA MPANGO WAO MAALUM.

 



Na,Jusline Marco,Matukio Daima Media ,Ngorongoro

Kamati tendaji ya Baraza la wafugaji wa Ngorongoro (Baraza la Wafugaji) wamekutana na uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kujadili na kupitisha orodha ya majina ya wanafunzi wa kidato cha tano wanaofadhiliwa na Mpango wa Mamlaka hiyo wataojiunga na vyuo vya Kati kwa mwezi septemba mwaka huu.


Akizungumza katika kikao hicho Kamishna wa Uhifadhi Ngorongoro Bw. Abdul-Razaq Badru amesema orodha ya majina hayo imepitishwa baada ya kujadiliwa katika ngazi ya Kijiji na Kata kisha kuwadilishwa kwenye Baraza hilo ikiwa ni miongoni mwa agenda zilizo jadiliwa katika kikao hicho ambacho kimelenga kuboresha huduma kwa jamii na kudumisha mahusiano kati ya wananchi walio ndani ya Hifadhi na NCAA.


Kwa mujibu wa Kamishna Badru, amesema kuwa agenda ya nyingine zilizojadiliwa katika kikao hicho ni kupitia taarifa za utekelezaji wa shughuli mbalimbali za miradi ikiwa ni pamoja na kupokea mapendekezo ya maeneo yanayopewa kipaumbele katika kuboresha miundombinu ya maji au kupeleka huduma ya maji ambapo amesema mpaka sasa tayari Mamlaka imepata mitambo ambayo itatumika katika uchimbaji wa visima 7 katika maeneo mbalimbali yaliyo ndani ya Hifadhi.


Ameongeza kuwa kikao hicho kimeunda Kamati ndogo kwa ajili ya kukamilisha tathimini ya kutizama namna bora ya kupanga vipaumbele vya kurekebisha maeneo ukorofi ya barabara zilizomo ndani ya Hifadhi pamoja na kukamilisha kalenda ya kufanya ukarabati kila mara kwenye maeneo hayo.


Sambamba na hayo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kukabiliana na masuala ya ulinzi, usalama na masuala ya taarifa zinazohusiana na wakazi pamoja na wageni wanaoingia ndani ya Hifadhi ikiwa ni pamoja na umuhimu wa ushirikishalwaji wa wanajamii kupitia serikali za vijiji, Kata na kwenye Baraza la ufugaji katika shughuli za uwekezaji zilizopo kwenye maeneo mbalimbali na zinazoendelea.


Kwa upande wake Edward Maura, Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji amesema lengo kuu la kikao hicho ni kupitisha wanafunzi hao ambao wanafadhiliwa na NCAA kupitia Baraza la Wafugaji kwenda kidato cha tano na watakao ingia kwenye vyuo vya Kati mwezi ujao ambapo jumla ya wanafunzi 33 wamepitishwa kutoka katika Kata 11 zenye vijiji 25.



Ameongeza kuwa Baraza hilo pamoja na Mamlaka ya Ngorongoro wamekubaliana kuendelea kulifanya maboresho ili kuhakikisha kwamba kutakuwepo na nyaraka ambazo zitaleta tija kwa jamii pamoja na kuweka mikakati mbalimbali ya namna ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi walio ndani ya Hifadhi hiyo.


Naye Katibu wa Baraza hilo James Moringe amesema kuwa ukaaji wa pamoja umeleta hisia ya Umoja na mshikamano baina ya watendaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na viongozi wa kijamii ambapo amempongeza Kamishna Badru kwa kusisitiza suala la kukaa pamoja katika utatuzi changamoto zilizopo.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI