Header Ads Widget

MERU FOREST YAGEUKA UWANJA WA MICHEZO NA UTALII


Arusha. Agosti 30, 2026. Zaidi ya wakimbiaji 700 kutoka ndani na nje ya Tanzania wamejitokeza katika msimu wa nne wa Meru Forest Adventure Race 2026, wakikimbia kwenye njia za kilomita 5, 10 na 20 ndani ya Shamba la Miti Meru-Usa, linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Arumeru mkoani Arusha.

Tofauti na mbio za kawaida zinazofanyika kwenye barabara za lami, washiriki walipita katika milima, mabonde, mito na njia za msituni, huku wakifurahia mandhari ya asili pamoja na maporomoko ya maji ya Napuru. Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Salum Kali, aliyeshiriki mbio za kilomita tano, alisema tukio hilo limeunganisha michezo, afya na utalii kwa namna inayowapa washiriki fursa ya kuyafahamu zaidi mazingira ya Tanzania.

Kali alisema Serikali inapaswa kuendelea kutumia michezo kama sehemu ya kukuza utalii wa ndani na kimataifa, akiwataka Watanzania kujitokeza kutembelea maeneo ya asili badala ya kusubiri wageni kutoka nje. Alisema mazingira ya Meru Forest, yanayopakana na maeneo ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha, yanaonyesha namna ambavyo michezo inaweza kuwa daraja la kuwatambulisha wananchi na wageni vivutio vya nchi.

Naye Mary Eliamani, mshiriki wa mbio hizo, alisema tukio hilo limempa fursa ya kujenga afya huku akifurahia mazingira ya msitu na maporomoko ya maji ya Napuru. Alisema kupitia mbio hizo, washiriki hawakufanya mazoezi pekee, bali walipata nafasi ya kujifunza na kufurahia uzuri wa eneo lililohifadhiwa.

Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Meru-Usa, Ernest Madata, alisema Meru Forest Adventure Race imekuwa ikifanyika tangu mwaka 2023 na mwaka huu imeongeza hamasa na idadi ya washiriki, huku takribani asilimia 70 ya waliojiandikisha wakiwa Watanzania. Alisema tukio hilo limefungua fursa za ajira na biashara kwa wananchi wanaouza vyakula, vinywaji na huduma mbalimbali, sambamba na kuongeza mapato ya Serikali kupitia usajili na viingilio.

Madata alisema Meru Forest ina vivutio vingi ikiwamo maporomoko ya maji ya Napuru, uoto wa asili, nyani na mandhari ya milima, huku eneo la uwekezaji likiwa na huduma na michezo mbalimbali kama zipline, malazi, chakula na vinywaji. Alisema matarajio ya msimu wa tano ni kuongeza idadi ya washiriki hadi zaidi ya 1,000, hatua itakayosaidia kuiweka Meru Forest katika ramani ya vivutio vinavyotumia michezo kukuza utalii.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Rogath Stephen Akhwari, alisema ushiriki wa wanariadha wa ndani na nje ya nchi umeifanya Meru Forest kuwa eneo muhimu la sport tourism na sport diplomacy. Alisema mazingira ya mwinuko wa takribani mita 2,200 kutoka usawa wa bahari yanatoa fursa muhimu kwa wanariadha, hasa wa mbio za masafa marefu, kutumia eneo hilo kwa mazoezi na maandalizi ya mashindano makubwa ya kimataifa.

Akhwari alisema michezo ya aina hiyo pia inasaidia kuitangaza Tanzania kwa wageni wanaoshiriki, huku akibainisha kuwa zaidi ya wanariadha 1,200 wa ndani na 166 kutoka mataifa mbalimbali walihusishwa na ushiriki wa mashindano hayo.














Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI