Na. Philipo Hassan - Dodoma
Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Mwishawa leo Agosti 31, 2026 amekielekeza Kitengo cha Mahusiano ya Jamii kuongeza wigo wa utoaji wa elimu ya uhifadhi kwa wananchi hususan jamii zinazozunguka Hifadhi za Taifa ili kuwawezesha wananchi hao kushiriki katika shughuli za uhifadhi na maendeleo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi cha Mwaka cha Kitengo cha Mahusiano ya Jamii cha TANAPA, kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi Kiunganishi TANAPA jijini Dodoma, Kamishna Mwishawa alieleza kuwa elimu ya uhifadhi ni muhimu katika kujenga uelewa na mahusiano mazuri kati ya Shirika na jamii.
“Ninasisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii ili kuwaelimisha wananchi namna ya kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji, kujikita kwenye shughuli za uzalishaji mali kupitia utalii pamoja na kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya ujirani mwema kwa kuhamasisha ushiriki wa vikundi mbalimbali vya kijamii,” alisema Kamishna Mwishawa.
Sambamba na hilo, Kamishna Mwishawa alieleza kuwa Kitengo cha Mahusiano ya Jamii kinapaswa kuwa kiunganishi kati ya TANAPA na jamii kutokana na kuwa na mahusiano ya moja kwa moja na wananchi, hivyo kina nafasi muhimu katika kuimarisha shughuli za uhifadhi, ulinzi na usalama wa watalii.
Kwa upande wake, Afisa Uhifadhi Mkuu na Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Uhifadhi, Glory Summay alibainisha kuwa kikao hicho ni muhimu katika kutathmini utekelezaji wa majukumu ya Kitengo cha Mahusiano ya Jamii, kubadilishana uzoefu uliopatikana, kubaini changamoto na kuweka mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati ya TANAPA na jamii zinazozunguka hifadhi.
“Kikao hiki kitatupa fursa ya kutathmini tulipofikia, kujifunza kutokana na uzoefu wetu na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha mahusiano na jamii kwa manufaa ya kuboresha maliasili katika Hifadhi za Taifa”, alieleza Mhifadhi Summay.
Kitengo cha Mahusiano ya Jamii kinatumia kikao hicho kuweka mikakati ya kuimarisha utendaji wa Kitengo, kuongeza maarifa na ujuzi wa utendaji kazi, hususan katika matumizi ya mfumo wa ukusanyaji taarifa, pamoja na kujengeana uelewa wa pamoja kuhusu mbinu bora za ushirikishwaji wa jamii kwa ajili ya kuboresha mahusiano na kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za uhifadhi.
Dhana ya ushirikishwaji wa jamii kwenye shughuli za uhifadhi ni jambo muhimu kwani Wananchi ndiyo msingi wa uhifadhi wa maliasili zilizopo. Ni dhahiri kuwa, uhifadhi hauwezi kufanikiwa kama jamii siyo sehemu ya uhifadhi huo.














0 Comments