Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Serbia kuongeza uwekezaji nchini Tanzania, akisisitiza kuwa wakati umefika kwa urafiki wa muda mrefu wa zaidi ya miongo sita kati ya Tanzania na Serbia kutafsiriwa katika biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi wenye matokeo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 31 Agosti 2026, jijini Belgrade, Serbia, alipozungumza katika mkutano na Chama cha Wafanyabiashara na Viwanda cha Serbia, ulioongozwa na Makamu wa Rais wa Chama hicho, Bw. Mihailo Vesović.
Amesema Tanzania ipo tayari kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kwa kuhamia zaidi katika miradi halisi ya biashara, uwekezaji, uzalishaji, uchakataji na ubia kati ya kampuni za Tanzania na Serbia.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema Tanzania Bara na Zanzibar zina fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta zikiwemo kilimo, madini, nishati, viwanda, miundombinu, utalii, Uchumi wa Buluu, viungo na mwani.
Amesema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao yakiwemo mahindi, alizeti, korosho na pamba, huku Zanzibar ikiwa na fursa kubwa katika uzalishaji wa viungo, mazao ya bustani na mwani. Amesisitiza kuwa fursa hizo zinahitaji uwekezaji katika uzalishaji, uchakataji na uongezaji thamani.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amesema Tanzania ina mahitaji makubwa ya bidhaa mbalimbali kutoka nje, ikiwemo mbolea, dawa, mafuta ya kula na ngano, ambazo Serbia ina uwezo wa kuzalisha, hivyo kuwepo kwa fursa ya kuongeza biashara na kuanzisha uzalishaji wa bidhaa hizo nchini Tanzania.
Katika sekta ya utalii, Dkt. Mwinyi amesema Tanzania Bara na Zanzibar zinaweza kuunganishwa katika safari moja ya watalii, ambapo wageni wanaweza kutembelea vivutio vya Serengeti na Mlima Kilimanjaro na kuhitimisha safari zao Zanzibar.
Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi ameahidi kuwa Serikali itafuatilia kwa karibu mapendekezo na fursa zitakazowasilishwa na wawekezaji wa Serbia, akisisitiza kuwa Tanzania iko tayari kwa biashara na uwekezaji wenye manufaa kwa pande zote.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesema Tanzania na Serbia zimekubaliana kuanzisha Tume ya Pamoja ya Uchumi, itakayoweka mfumo wa kushughulikia na kukuza masuala ya biashara, uwekezaji, huduma za kifedha na maeneo mengine ya ushirikiano wa kiuchumi.
Amesema Serikali pia imewasilisha kwa Chama cha Wafanyabiashara na Viwanda cha Serbia taarifa za miradi na fursa mbalimbali za uwekezaji nchini Tanzania, kwa lengo la kuzifikisha kwa kampuni za Serbia zenye nia ya kuwekeza na kujenga ubia na wafanyabiashara wa Tanzania.
















0 Comments