Header Ads Widget

MAKALA:NaCoNGO MKOMBOZI WA MAENDELEO MUFINDI


-NGOs  68 zaongeza nguvu katika afya, elimu, maji na uchumi 

-Zachangia Miradi ya maendeleo kwa zaidi Tsh bilioni 15 kwa mwaka .

-Serikali yataka uwazi na uratibu, huku Water for Africa na World Vision zikiongeza kasi ya miradi
Mkuu wa wilaya ya Mufindi Dkt Linda Selekwa (aliyekaa katikati) akiwa na viongozi wa NaCoNGo Mufindi na waratibu wa Jukwaa hilo kwa mwaka huu Shirika la World Vision na wa kwanza kushoto ni meneja wa shirika la Water For Afrika Nestry Sanga picha na Matukio Daima Media


NA FRANCIS GODWIN , MUFINDI

MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali yameendelea kuwa nguzo muhimu katika kuchochea maendeleo katika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, yakishirikiana na Serikali kutekeleza miradi ya afya, elimu, maji, kilimo, mifugo, miundombinu, uchumi wa kaya na ustawi wa jamii.


Mchango huo umejitokeza katika Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali(NaCoNGO) wilaya ya Mufindi mkoani Iringa  lililofanyika ukumbi wa Mbalamaziwa ambalo limewakutanisha viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, madiwani, wenyeviti wa vijiji na wananchi  mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.


Jukwaa hilo limekuwa sehemu ya wadau kutathmini mafanikio, changamoto na mwelekeo wa shughuli za mashirika, huku msisitizo mkubwa ukiwekwa katika uwazi, uwajibikaji, ushirikiano na Serikali pamoja na kutafuta njia mpya za kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa endelevu.


Wilaya ya Mufindi ina jumla ya mashirika 68 yaliyosajiliwa, ambapo 65 yanaendelea kufanya kazi. Katika mwaka wa fedha 2025/2026 pekee, mashirika hayo yameelezwa kuwafikia zaidi ya wananchi 48,000 kupitia afua mbalimbali za maendeleo.
Mkuu wa wilaya ya Mufindi Dkt Linda Selekwa akimkabidhi cheti cha pongezi mkurugenzi wa shirika la Rural Development Organization (RDO) na Mwenyekiti wa NaCoNGo Wilaya ya Mufindi Fidelis Filipatali  


Mwenyekiti wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Iringa na Mjumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Fidelis Filipali, amesema mashirika hayo yamekuwa yakitoa mchango mkubwa katika maeneo mbalimbali, lakini wakati umefika kwao kujenga mifumo itakayowezesha shughuli zao kuendelea hata baada ya ufadhili wa miradi kumalizika.

Amesema kaulimbiu ya “Fikra mpya kuhusu maendeleo ya mashirika yasiyo ya kiserikali” inalenga kuhamasisha mashirika kutafuta vyanzo vya mapato na kupunguza utegemezi mkubwa kwa wafadhili.

Kwa mujibu wa Filipali, mashirika yanapaswa kuwa na mifumo ya kuzalisha mapato huku yakizingatia uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha, jambo litakalosaidia kulinda uendelevu wa miradi na kuongeza uwezo wa taasisi hizo kuwahudumia wananchi.

Amesema pia Mufindi imeanza kubadili mfumo wa uratibu wa mashirika kwa kupunguza utegemezi wa mikutano ya ofisini na badala yake viongozi na wadau kutembelea miradi moja kwa moja katika maeneo inakotekelezwa.

Ziara hizo zinahusisha viongozi kuanzia ngazi ya kijiji, kata, tarafa hadi wilaya, pamoja na madiwani, hatua inayowezesha Serikali na mashirika kuona hali halisi ya miradi, mafanikio yake na changamoto zinazohitaji ufumbuzi.

Utaratibu huo pia umetoa nafasi kwa mashirika makubwa na madogo kujifunza kutoka kwa wenzao na kutafuta suluhisho la pamoja kwa changamoto zinazojitokeza.
TAZAMA VIDEO YA MWENYEKITI NACONGO BOFYA LINK HII

Anasema NaCoNGO Mufindi ipo kutekeleza Dira 2050 na kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kulitumikia Taifa ndio maana  Kaulimbiu ya NaCoNGO Mufindi "Fikra Mpya Kuhusu uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha Kupitia Vyanzo vya ndani.


Hata hivyo Fidelisi ambae ni mkurugenzi wa shirika la Rural Development Organization (RDO) ametaja mchango wa shirika lake kwa mwaka katika maendeleo ya Mufindi kwenye hufuma mbali mbali kama maji,elimu na nyingine kuwa ni zaidi ya Tsh bilioni 3 na hivyo kufikisha kiasi cha Tsh Bilioni 15 ambacho kimechangiwa na mashirika yote ndani ya wilaya ya Mufindi kwa mwaka .

DC SELEKWA: SHIRIKIANENI NA IDARA ZA SERIKALI

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Selekwa, ameyapongeza mashirika yasiyo ya kiserikali kwa mchango wao katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha huduma za wananchi.

Amesema uwepo wa mashirika hayo umeongeza nguvu katika utekelezaji wa miradi ya afya, elimu, maji, miundombinu na sekta nyingine, lakini akasisitiza umuhimu wa kila shirika kushirikiana kwa karibu na idara husika za Serikali.TAZAMA MSISITIZO WA DC LINDA BOFYA HAPA

Kwa mujibu wa Dkt. Selekwa, uratibu huo ni muhimu ili kuzuia hali ya miradi mingi kuelekezwa katika eneo moja wakati maeneo mengine yenye mahitaji makubwa yakibaki nyuma.

Amesisitiza kuwa miradi ya afya inapaswa kuratibiwa na idara ya afya, huku miradi ya maji, elimu na sekta nyingine ikihusisha wataalamu husika ili mipango inayotekelezwa iendane na vipaumbele vya wilaya na mahitaji halisi ya wananchi.

Katibu wa NaCoNGO Wilaya ya Mufindi, Marco Shayo, amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, mashirika hayo bado yanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kutokuwa na ofisi rasmi ya kuratibu shughuli zao na upungufu wa fedha za kuendeleza miradi baada ya wafadhili kumaliza kipindi cha ufadhili.

Amesema baadhi ya miradi, ikiwemo iliyolenga kuboresha miundombinu ya shule za msingi, bado inahitaji matengenezo na uwekezaji zaidi ili manufaa yaliyopatikana yaendelee kuwafikia wananchi.

WATER FOR AFRICA YAPUNGUZA KERO YA MAJI

Miongoni mwa mashirika yaliyotajwa kuwa na mchango mkubwa Mufindi ni Water for Africa, ambalo limekuwa likichimba visima katika vijiji, shule, vituo vya afya na maeneo ya makazi yenye changamoto ya maji.


Katibu wa Mbunge wa Mufindi Kusini, Aida Kaduma, amesema shughuli za Water for Africa zimechangia kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama, hususan katika maeneo yaliyokuwa yakikabiliwa na ukame na uhaba wa vyanzo vya uhakika vya maji.

Ametaja Kata ya Ihowanza kuwa miongoni mwa maeneo yaliyokuwa na changamoto kubwa, akisema uchimbaji wa visima umeanza kupunguza adha iliyokuwa ikiwakabili wananchi.

Kaduma amepongeza Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira yanayoruhusu mashirika yasiyo ya kiserikali kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto za wananchi.

Amesema Mbunge wa Mufindi Kusini, David Kienzile, pia amekuwa akishirikiana na wadau hao kwa kuwaelekeza katika maeneo yenye mahitaji makubwa, ili miradi iweze kuwafikia wananchi wanaohitaji huduma zaidi.


Meneja wa Water for Africa Tanzania, Nestory Sanga, amesema shirika hilo limejikita kusaidia jamii kuondokana na adha ya maji kwa kutekeleza miradi katika shule, hospitali, vijiji na maeneo mengine.

Amesema lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa urahisi na kwa gharama nafuu, huku shirika likiendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha huduma hiyo muhimu.TAZAMA VIDEO YA WATER FOR AFRIKA BOFYA HAPA

WORLD VISION YATENGA ZAIDI YA SH BILIONI 4.6

Wakati Water for Africa ikiongeza nguvu katika sekta ya maji, World Vision Tanzania imetenga Dola za Marekani milioni 1.8, sawa na zaidi ya Sh bilioni 4.6, kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Iringa kwa mwaka wa fedha 2026.

Fedha hizo zimepangwa kutumika kupitia Area Programmes za Nyololo, Malangali na Idumbala, zikilenga kuboresha maisha ya watoto, familia na jamii.

Nyololo Area Programme imetengewa Dola 826,743, sawa na takribani Sh bilioni 2.17, Malangali AP Dola 471,627, sawa na takribani Sh bilioni 1.22, huku Idumbala AP ikitengewa Dola 494,232, sawa na takribani Sh bilioni 1.28.

Kwa ujumla, programu hizo tatu zina bajeti ya Dola 1,802,602, sawa na takribani Sh bilioni 4.68.

Fedha hizo zitaelekezwa katika elimu, kilimo na mifugo, afya na lishe, maji na usafi wa mazingira, uchumi wa kaya pamoja na ulinzi na usalama wa mtoto.



Asilimia 70 ya bajeti, sawa na takribani Sh bilioni 3.28, imepangwa kwenda moja kwa moja katika utekelezaji wa shughuli za miradi, wakati asilimia 30, takribani Sh bilioni 1.4, ikielekezwa katika uendeshaji na shughuli za utawala.

World Vision Tanzania ilianza shughuli zake Mkoa wa Iringa mwaka 2019 kupitia Wilaya ya Iringa na kupanua huduma zake Mufindi mwaka 2020.

Kwa sasa inaendesha Area Programmes tano ambazo ni Wasa, Kihanga, Nyololo, Idumbala na Malangali. 


Miradi hiyo inafikia maeneo ya tarafa za Kiponzelo na Malangali katika kata za Wasa, Lumuli, Kihanga, Maboga, Nyololo, Maduma, Mbalamaziwa, Idunda, Malangali na Ihowanza.

Katika mpango wake wa kimkakati wa miaka mitano wa 2026–2030, World Vision Tanzania inalenga kuwafikia watoto milioni 3.4 kupitia programu zake nchini.

JAMII YASHIRIKISHWA KUCHAGUA VIPAUMBELE

Kaimu Meneja wa World Vision Kanda ya Kati na Kusini, Zakaria Shibukulu, amesema shirika hilo linatumia mfumo wa ushirikishwaji wa wananchi katika kubaini changamoto na kupanga vipaumbele vya miradi.


Amesema kupitia mfumo wa community budget, wananchi hupewa nafasi ya kueleza changamoto zinazowakabili, waarna kamati za uratibu huchambua mahitaji hayo na kuamua maeneo ya kupewa kipaumbele kulingana na ukubwa wa tatizo na rasilimali zilizopo.

“Rasilimali siku zote hazitoshi, kwa hiyo lazima tufanye uchaguzi. Sehemu ambayo changamoto ni kubwa zaidi ndiyo tunaanza nayo kulingana na rasilimali tulizonazo,” amesema Shibukulu.

Kwa mwaka unaoishia, amesema World Vision imetumia takribani Sh bilioni 3.7 katika Wilaya ya Mufindi kupitia miradi ya elimu, afya na lishe, maji na usafi wa mazingira, kilimo na mifugo pamoja na ulinzi na usalama wa mtoto.

Hata hivyo, shirika hilo limebainisha kuwa mahitaji ya jamii bado ni makubwa kuliko rasilimali zinazopatikana. 


Changamoto nyingine ni ushiriki mdogo wa vijana, hasa walio nje ya mfumo rasmi wa elimu, katika baadhi ya shughuli za miradi.

Hali hiyo inaonyesha umuhimu wa Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi na wananchi kuendelea kujenga ushirikiano wenye uwazi na uwajibikaji.

Kwa Mufindi, mchango wa mashirika hayo hauishii katika fedha pekee, bali unaonekana katika visima vinavyotoa maji, miundombinu ya shule, huduma za afya, miradi ya kilimo na mifugo na programu za ulinzi wa watoto.


Kadiri mahitaji ya wananchi yanavyoendelea kuongezeka, changamoto kubwa sasa ni kuhakikisha mafanikio ya miradi hiyo yanadumu. 

Makala haya yameandaliwa na Francis Godwin ,Matukio Daima Media karibu kutangaza nasi piga simu  0754026299







Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI