Na Matukio DaimaMedia
Msanii maarufu wa muziki wa Gospel kutoka Nigeria, Moses Bliss, amewasili nchini Tanzania kwa mara ya kwanza tayari kushiriki katika Tamasha la The Rising Fest linalotarajiwa kufanyika kesho, Agosti 15, 2026, katika Viwanja vya Lugalo Golf Club jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili nchini, Moses Bliss amesema amefurahishwa na mapokezi aliyoyapata, akieleza kuwa amejisikia kama yupo nyumbani.
Amesema anaamini tamasha hilo litakuwa jukwaa la kipekee la ibada na kumtukuza Mungu, huku akitarajia washiriki kupata baraka, faraja na ushuhuda kupitia tukio hilo.
“”Nimefurahi sana kuwa Tanzania. Mapokezi niliyoyapata yamenifanya nijisikie kama niko nyumbani,” amesema.Kwa upande wake, mmoja wa waandaaji wa tamasha hilo, Carolyn Claire, amesema The Rising Fest imeanzishwa kama jukwaa la kuunganisha watu kupitia imani, likiwaleta pamoja watu kutoka nyanja mbalimbali za jamii.
Amesema tamasha hilo linalenga pia kupanua mtazamo kuhusu muziki wa Gospel kwa kuonyesha namna imani inavyoweza kuhusishwa na vipaji, familia, biashara na maendeleo ya jamii.
Kwa mujibu wa Carolyn, tamasha hilo litahusisha shughuli mbalimbali zitakazowalenga watoto, vijana na jamii kwa ujumla, zikiwemo maonesho ya vipaji, muziki, dansi na shughuli nyingine za ubunifu.
The Rising Fest pia inalenga kutumia sanaa na imani kama njia ya kuunganisha jamii na kutoa nafasi kwa watu mbalimbali kuonyesha vipaji muziki, dansi na shughuli za ubunifu.










0 Comments