Na Matukio Daima Media ,NJOMBE
KAMATI Tendaji ya Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) Taifa imehitimisha kikao kazi chake kwa kufanya ziara ya mafunzo katika shamba la Mkulima Bora wa Zao la Parachichi kitaifa, Abishae Hairun Mwalongo, lililopo Kijiji cha Igosi, Wilaya ya Wanging’ombe, mkoani Njombe.
Ziara hiyo, iliyoongozwa na Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Mhe. Agnetha Mpangile, imelenga kuwawezesha wajumbe wa kamati hiyo kujifunza kwa vitendo kuhusu kilimo cha parachichi na namna wakulima wanavyoweza kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao.
Mwalongo, ambaye ni mmiliki wa MWIDIS Green Garden, aliwaeleza wajumbe hao hatua mbalimbali za kilimo cha parachichi, kuanzia uchaguzi wa mbegu bora, maandalizi ya shamba, upandaji hadi namna ya kulitunza shamba katika vipindi tofauti vya mwaka.
Alisema matumizi ya mbegu bora pamoja na maandalizi sahihi ya shamba ni miongoni mwa mambo muhimu yanayomwezesha mkulima kupata mavuno yenye tija na mazao yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko.
Katika ziara hiyo, Mwalongo pia alitoa maelekezo kuhusu aina mbalimbali za mbegu bora za parachichi na namna ya kuzitumia kulingana na mazingira ya eneo husika.
Alisema wakulima wanapaswa kuzingatia utaalamu katika kila hatua ya uzalishaji ili kuongeza tija na kuhakikisha zao hilo linakuwa na ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mwalongo aliwashukuru viongozi wa ALAT Taifa kwa kutenga muda na kufika katika shamba lake kwa lengo la kujifunza na kuona kwa vitendo namna kilimo cha parachichi kinavyofanyika.
Alisema ziara hiyo ni muhimu kwa kuwa inatoa fursa kwa viongozi kujionea shughuli za kilimo na kupata uelewa wa changamoto na fursa zinazowakabili wakulima.
Kwa upande wake, ziara hiyo imekuwa sehemu ya shughuli za Kamati Tendaji ya ALAT Taifa mkoani Njombe, ikiwa ni hatua ya kuunganisha masuala ya utawala wa Serikali za Mitaa na shughuli za kiuchumi zinazofanywa na wananchi katika maeneo yao.
Njombe ni miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri katika uzalishaji wa parachichi nchini, hivyo ziara hiyo imeongeza fursa ya kubadilishana uzoefu kuhusu namna ya kuimarisha kilimo na kuongeza tija kwa wakulima.










0 Comments