Na Mwandishi Wetu.
Dar es Salaam, Julai 3, 2026 – Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limeendelea kuthibitisha ubora wake katika uzalishaji na maendeleo ya uchumi baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika masuala ya uzalishaji pamoja na shughuli za kilimo na uvuvi kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) 2026.
Tuzo hiyo ilitolewa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na kukabidhiwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni kutambua mchango mkubwa wa JKT katika uzalishaji, kilimo, uvuvi na maendeleo ya viwanda nchini.Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maonesho ya Sabasaba Kitaifa kwa Jeshi la Kujenga Taifa, Brigedia Jenerali Shija Lupi, alisema ushindi huo ni heshima kubwa kwa JKT na umeongeza hamasa ya kuendelea kufanya kazi kwa ubunifu na weledi.
"Leo tumepokea tuzo kutoka TanTrade. Tuzo hii ni kubwa sana na imetupa hamasa kubwa kwa sababu tumekuwa washindi wa kwanza katika masuala ya uzalishaji pamoja na shughuli za kilimo na uvuvi," alisema Brigedia Jenerali Lupi.Alieleza kuwa mafanikio hayo si ya bahati mbaya, bali ni mwendelezo wa rekodi nzuri ambayo JKT imekuwa ikiionesha katika maonesho ya Sabasaba kwa miaka mbalimbali.
Kwa mujibu wake, mwaka uliopita JKT pia ilifanya vizuri katika kundi la Interior Design, ikionesha umahiri katika utengenezaji wa samani (furniture) na mapambo ya ndani (interior decoration), sambamba na kung'ara katika bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na viwanda vya JKT.
"Tunamshukuru Mungu na tunaendelea kuthibitisha kuwa JKT ni bingwa katika nyanja mbalimbali za uzalishaji. Haya ni matokeo ya juhudi, ubunifu na kazi kubwa inayofanywa na vijana pamoja na watumishi wetu," aliongeza.
Ushindi huo unaendelea kuimarisha nafasi ya Jeshi la Kujenga Taifa kama taasisi muhimu katika kukuza uzalishaji wa ndani, kuongeza thamani ya bidhaa, kuendeleza sekta za kilimo na uvuvi, pamoja na kuchochea maendeleo ya viwanda na uchumi wa Tanzania.Kwa mafanikio hayo, JKT imeendelea kuwa mfano wa taasisi inayotekeleza kwa vitendo falsafa ya kujitegemea kupitia uzalishaji, huku ikiendelea kuonesha uwezo wake wa kushindana na kuibuka kinara katika maonesho makubwa ya biashara nchini.








0 Comments