Header Ads Widget

WENYE MDOMO WAZI KUTIBIWA BURE MUHIMBILI



Na. Mwandishi Wetu,


HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH), kwa kushirikiana na Shirika la Smile Train Tanzania, inaendelea kutoa huduma za uchunguzi, upasuaji na matibabu bila malipo kwa watoto na watu wazima wenye changamoto ya mdomo wazi na kaakaa wazi, huku ikiwahimiza wananchi kujitokeza kupata huduma hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Rachel Mhavile Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, amesema wagonjwa kutoka maeneo yote nchini watapokelewa, na wale wasioweza kufika hospitalini watawezeshwa kufikishwa Muhimbili na kurejeshwa makwao baada ya matibabu kwa gharama za hospitali. Ameongeza kuwa wazazi au walezi wanapaswa kuwasiliana kupitia namba 0790 312 335 ili kuanza utaratibu wa kupata huduma.

Dkt. Mhavile amesema takwimu zinaonyesha watoto wengi huzaliwa na changamoto ya mdomo wazi na kaakaa wazi kila mwaka nchini, hivyo Muhimbili imeweka mfumo wa huduma jumuishi unaohusisha wataalamu wa upasuaji, lishe, tiba ya usemi na fani nyingine ili kuhakikisha mgonjwa anapata matibabu yote muhimu katika eneo moja hadi anapopona.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Smile Train Tanzania, Veronica Kamwela amesema watoto na watu wazima ambao hawajawahi kufanyiwa upasuaji wa mdomo wazi au kaakaa wazi wanakaribishwa Muhimbili kupata matibabu bila malipo, akisisitiza kuwa shirika hilo limejipanga kugharamia wagonjwa wote watakaofika bila kuweka ukomo wa idadi yao.

Muhimbili imewahimiza Watanzania kutoa taarifa wanapowaona watoto au watu wazima wenye changamoto ya mdomo wazi na kaakaa wazi ili waelekezwe hospitalini mapema, hatua itakayowasaidia kupata matibabu kwa wakati na kuboresha afya pamoja na ubora wa maisha yao.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI