Header Ads Widget

TRA YATAKIWA KUIMARISHA USIMAMIZI WA KODI BAADA YA HOJA ZA UKAGUZI WA SERIKALI

 

Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma

UFANISI wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali umeingia kwenye mjadala mpya bungeni baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuishauri Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuimarisha mifumo yake ya usimamizi wa kodi ili kupunguza mapungufu yaliyojitokeza katika ukaguzi wa hesabu za Serikali.

Kamati hiyo imebaini kuwa baadhi ya hoja zilizoainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2025 zinahitaji hatua za haraka ili kuimarisha uwazi, usahihi na ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Akizungumza katika majumuisho ya kikao kati ya PAC na uongozi wa TRA, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe Devotha Minja, amesema ni muhimu taasisi hiyo kuhakikisha mifumo ya ukaguzi wa kodi inaimarishwa ili kuondoa mianya inayoweza kusababisha upotevu wa mapato ya Serikali.


Kamati hiyo pia imeelekeza kuongezwa kwa weledi katika uhakiki wa walipa kodi, ufuatiliaji wa mapato pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali inayowezesha ufuatiliaji wa makusanyo kwa wakati halisi.


Kwa upande wa TRA, Kamishna Mkuu Yusuph Mwenda amesema mamlaka hiyo imepokea maelekezo ya kamati na imeanza kuweka mikakati ya kuyafanyia kazi kwa lengo la kuboresha utendaji na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.


Alisema TRA itaendelea kufanya maboresho ya mifumo yake ya ndani ili kuhakikisha mapato ya Serikali yanaongezeka sambamba na kuboresha huduma kwa walipa kodi nchini.


Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TRA, Uledi Mussa, amesema majadiliano hayo yamekuwa chachu ya kuibua maeneo mapya ya maboresho, hususan katika usimamizi wa kodi na utoaji wa huduma kwa wananchi.


Aidha, amesisitiza kuwa uhamasishaji wa ulipaji kodi kwa hiari bado ni nguzo muhimu katika kupanua wigo wa mapato ya Serikali na kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


Kikao hicho kimeendelea kuonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Bunge na taasisi za Serikali katika kuhakikisha uwajibikaji unaimarishwa na rasilimali za taifa zinasimamiwa kwa ufanisi.


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI