Header Ads Widget

NSSF YAHAMASISHA WABUNGE KUWA MABALOZI WA HIFADHI YA JAMII KWA WALIOJIAJIRI

Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umewataka Waheshimiwa Wabunge kutumia nafasi zao za uongozi kuwahamasisha wananchi, hususan wale wanaojiajiri, kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kujenga usalama wa maisha yao ya sasa na ya baadaye.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, ambaye amesema bado kuna idadi kubwa ya wananchi wanaofanya shughuli mbalimbali za kiuchumi katika sekta isiyo rasmi lakini hawajanufaika ipasavyo na huduma za hifadhi ya jamii, licha ya mchango wao mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa.

Amesema kuongezeka kwa ushiriki wa wananchi katika mifuko ya hifadhi ya jamii kutasaidia kuimarisha ustawi wa jamii, kupunguza umaskini wa kipato na kuongeza uwezo wa wananchi kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha wanapofikia uzee au wanapokumbwa na majanga yanayoathiri shughuli zao za kiuchumi.

“Mifuko ya hifadhi ya jamii ni nguzo muhimu katika kujenga uchumi jumuishi unaowajali wananchi wa makundi yote tunahitaji ushirikiano wa wabunge ili ujumbe huu uwafikie wananchi wengi zaidi, hasa wale wanaojiajiri,” amesema Mshomba.

Akizungumza katika mafunzo maalumu kwa Waheshimiwa Wabunge yaliyofanyika Juni 15, 2026, katika Ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni Dodoma, Mshomba amesema wabunge wana nafasi ya kipekee ya kuhamasisha wananchi katika maeneo yao kuhusu umuhimu wa kujiwekea kinga ya kiuchumi kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na NSSF pamoja na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), yakilenga kuwajengea wabunge uelewa kuhusu mpango wa kuwajumuisha wananchi waliojiajiri katika mifuko ya hifadhi ya jamii.

Katika mafunzo hayo, wabunge walipata fursa ya kufahamu kwa kina Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi Waliojiajiri, ambayo imeundwa mahsusi kuwapatia wananchi wanaojitafutia kipato katika sekta isiyo rasmi fursa ya kupata mafao na huduma za hifadhi ya jamii.

Mshomba ameeleza kuwa skimu hiyo inawahusu wananchi wanaofanya shughuli mbalimbali za kujiajiri ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji mdogo wa madini, biashara ndogondogo, ubodaboda, umachinga, sanaa na shughuli nyingine za uzalishaji mali.

Makundi mengine yanayonufaika ni pamoja na mama lishe, baba lishe, wasusi, wachuuzi wa masokoni pamoja na wafanyabiashara wadogo na wa kati ambao kwa miaka mingi wamekuwa uti wa mgongo wa uchumi wa taifa.

Amefafanua kuwa ili mwananchi aweze kujiunga na skimu hiyo anatakiwa kuwa Mtanzania mwenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 70, mkazi wa Tanzania Bara, asiwe mnufaika wa pensheni kutoka mfuko mwingine wa hifadhi ya jamii na awe anajishughulisha na shughuli za kujiajiri.

Aidha, amesisitiza kuwa kuimarika kwa wigo wa hifadhi ya jamii kutaleta manufaa makubwa kwa wananchi mmoja mmoja na kwa taifa kwa ujumla, kwani kutajenga jamii yenye uhakika wa kipato, ustawi wa maisha na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiuchumi katika hatua mbalimbali za maisha.

Mshomba amesema kwa kuwataka wabunge kuwa mabalozi wa mabadiliko hayo kwa kuendelea kuelimisha wananchi katika majimbo yao kuhusu umuhimu wa kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma katika safari ya kuelekea maendeleo jumuishi.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI