Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema takwimu rasmi zitakuwa nyenzo muhimu katika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuifikisha Tanzania katika uchumi wa dola trilioni moja na kuongeza kipato cha wananchi.
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa NBS, Daniel Masolwa, alisema hayo wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma, ambapo taasisi hiyo inashiriki kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma na majukumu yake.
Masolwa alisema kaulimbiu ya mwaka huu inayosema “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu” imeipa NBS fursa ya kueleza umuhimu wa takwimu rasmi katika kupanga maendeleo, kufanya maamuzi sahihi na kufuatilia utekelezaji wa mipango mbalimbali ya taifa.
Amrsema kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu, Sura ya 351, NBS imepewa mamlaka ya kukusanya, kuchakata na kusambaza takwimu rasmi zinazotumika katika sekta mbalimbali za maendeleo.
“Takwimu rasmi ni msingi wa upangaji wa maendeleo. Serikali, sekta binafsi, watafiti na wadau wengine hutegemea takwimu hizi katika kufanya maamuzi na kupima matokeo ya mipango inayotekelezwa,” alisema.
Masolwa alitaja baadhi ya takwimu zinazozalishwa na NBS kuwa ni pamoja na takwimu za mfumuko wa bei zinazotolewa kila mwezi na kuonesha mwenendo wa bei za bidhaa na huduma nchini.
Pia amesema ofisi hiyo huzalisha takwimu za Pato la Taifa kwa vipindi vya robo mwaka ambazo huonesha thamani ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini, kiwango cha ukuaji wa uchumi na mchango wa kila sekta katika uchumi wa taifa.
Ameongeza kuwa NBS pia hutoa takwimu za ajira zinazoonesha hali ya soko la ajira, kiwango cha ukosefu wa ajira, watu waliopo katika ajira pamoja na wale waliopo nje ya nguvu kazi.
“Tunaendelea kuzalisha pia takwimu za kilimo, uzalishaji viwandani, biashara ya nje, pamoja na takwimu za kijamii zinazotokana na Sensa ya Watu na Makazi ambazo zinaonesha mwenendo wa idadi ya watu, mgawanyo wa umri na rasilimali watu iliyopo nchini,” amesema.
Masolwa alisema takwimu hizo ni muhimu katika kukokotoa viashiria mbalimbali vya maendeleo ikiwemo wastani wa pato la mwananchi na hali ya uchumi kwa ujumla.
Akizungumzia Dira 2050, alisema mafanikio ya utekelezaji wake yatategemea uwezo wa nchi kutumia takwimu katika kupanga, kufuatilia na kutathmini hatua zinazopigwa kuelekea malengo yaliyowekwa.
“Lengo la Dira 2050 ni kuwa na uchumi mkubwa zaidi unaotoa ustawi kwa wananchi ili kufikia malengo hayo tunahitaji jamii inayojifunza, inayozalisha maarifa, inayotumia ujuzi na inayofanya maamuzi kwa kuzingatia takwimu sahihi,” amesema.
Amesisitiza kuwa NBS itaendelea kuhakikisha takwimu rasmi zinapatikana kwa wakati na kwa ubora unaohitajika ili kusaidia juhudi za maendeleo ya taifa katika kipindi chote cha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mwisho






0 Comments