Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imetunukiwa Tuzo ya Heshima ya Mafanikio katika Sekta ya Afya na Famasi kwenye Tuzo za Biashara na Ubunifu Zanzibar 2026, zilizofanyika usiku wa Juni 27, 2026, visiwani Zanzibar.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Delilah Kimambo amesema tuzo hiyo ni heshima kwa wataalamu wa afya wote nchini wanaotoa huduma kwa kujituma, uadilifu na uzalendo katika kuboresha maisha ya wananchi.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya wataalam wa afya, uongozi wa taasisi na wadau mbalimbali wa sekta ya afya, wanaoendelea kuiunga mkono hospitali hiyo na kusisitiza kuwa Muhimbili itaendelea kuimarisha huduma za ubingwa na ubingwa bobezi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na zinazokidhi viwango vya kimataifa.
Muhimbili imeibuka mshindi baada ya kushindana na taasisi nyingine tano, hatua inayoonesha kutambuliwa kwa mchango wake katika kuimarisha huduma za afya na kuboresha ubora wa matibabu nchini. Ushindi huo pia unaakisi jitihada zake katika kuongeza viwango vya huduma na kuimarisha huduma za ubingwa na ubingwa bobezi.
Tuzo za Biashara na Ubunifu Zanzibar 2026 ni sehemu ya maonesho ya biashara na uwekezaji yanayofanyika visiwani Zanzibar, yakilenga kutambua na kuthamini taasisi, kampuni na watu binafsi wanaochangia katika kukuza uchumi kupitia ubunifu na utoaji wa huduma bora. Tuzo hizi huwakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi, zikiwa jukwaa la kuhamasisha ushindani, ubunifu na maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.









0 Comments