Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba ameagiza kuanza mara moja ujenzi wa barabara za Nyololo-Mtwango na Mafinga-Mgololo katika Jimbo la Mufindi Kusini, akisisitiza kuwa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan hayapaswi kucheleweshwa bali kutekelezwa kwa haraka.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Igowole mkoani Iringa, amesema Serikali inaendelea kutekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo na kwamba Rais ameonyesha mfano wa uongozi wa matokeo kupitia kazi zake.
Katika kuharakisha mradi wa barabara ya Nyololo-Mtwango, ameiagiza TANROADS Mkoa wa Iringa kuhakikisha mkandarasi anapatikana ndani ya wiki mbili ili ujenzi uanze bila urasimu au kucheleweshwa.
Aidha, kuhusu barabara ya Mafinga-Mgololo, amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuwasiliana mara moja na Wizara ya Fedha ili kupata fedha za awali (advance payment) na kuhakikisha mradi unaanza mara moja.
Waziri Mkuu pia alishughulikia malalamiko ya wananchi dhidi ya kampuni ya Leshenia Investment kwa madai ya kutolipa haki zao, akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia unyanyasaji na kucheleweshwa kwa malipo halali.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mufindi Kusini David Mwakiposa Kihenzile amesema changamoto ya barabara imekuwa kikwazo kikubwa kwa shughuli za kiuchumi, hususan usafirishaji wa mazao ya wakulima na upatikanaji wa malighafi viwandani.







0 Comments