Na Hamida Ramadhan, Matukio, Daima Media Dodoma
WAFANYABISHARA zaidi ya 300 wa Soko la Rehema Nchimbi jijini Dodoma, waliohamishwa baada ya eneo hilo kuchukuliwa na Bunge Oktoba mwaka jana, wameuomba uongozi wa Jiji la Dodoma kuondoa zuio la kuendesha biashara katika eneo mbadala la Umoga walilopewa na Waziri Mkuu.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti katika eneo la Umonga, baadhi ya wafanyabiashara hao wamesema ni zaidi ya miezi saba sasa hawajafanya biashara yoyote, hali inayochangia ugumu wa maisha yao.
Prisca Chibwaye, mmoja wa wafanyabiashara hao, amesema tangu walipoondolewa kwenye eneo lao la awali wamekuwa wakifuatilia kupata eneo mbadala bila mafanikio.
“Mwaka jana tuliondolewa kwenye vibanda vyetu vya biashara bila kupewa taarifa wala fidia baada ya Bunge kuchukua eneo lile lakini tunashukuru serikali kupitia mkuu wa mkoa alisimamia tukaletwa katika eneo hili la Umonga lakini jiji hawataki tufanye biashara hapa,” amesema.
Ameongeza kuwa Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba alipofanya ziara kwenye Soko la Machinga mapema mwaka huu alitoa maagizo kuwa wafanyabiashara wote walihamishwa kutoka Soko la Rehema Nchimbi wahamishiwe eneo la Umoga.
“Waziri Mkuu ametoa maagizo wote tulihamishwa tuliletwe hapa Umoga na akaagiza eneo hili lijazwe kifusi ili kuzuia maji kujaa wakati wa mvua na liwe eneo la kudumu lakini hadi leo hakuna kilichofanyika,” amesema.
Aidha amesema kutokana na hali hiyo wamekuwa wakikaa muda mrefu bila kufanya biashara hali inayoendelea kuongeza ugumu wa maisha kwa familia zao.
Amesema wafanyabiashara wengi wana mikopo kutoka taasisi za kifedha hivyo wamelazimika kuuza vitu vya ndani ili kurejesha mikopo hiyo.
“Tuna mikopo lakini pia tunasomesha watoto wanahitaji kula na biashara ndiyo tegemeo letu lakini ni miezi saba sasa hatujafanya biashara maisha yazidi kuwa magumu kila siku,” amesema.
Ameongeza kuwa wanaomba serikali kuingilia kati ili waruhusiwe kutumia eneo hilo na kuanza tena biashara zao kama ilivyokuwa awali.
Katibu wa Bodi ya Wadhamini wa soko hilo, Abdullah Gogo, ameekezawamekuwa wakipitia changamoto tangu kufungwa kwa soko hilo Oktoba 29 mwaka jana bila kupatiwa notisi ya kuondolewa.
Amesema kufungwa kwa soko hilo kumeathiri zaidi ya wafanyabiashara 300 waliokuwa wakitegemea eneo hilo kwa kipato cha kila siku.
Hata hivyo amesema hawana tatizo na Ofisi ya Bunge, bali changamoto kubwa ipo katika utekelezaji wa maamuzi yaliyotolewa kuhusu kupatiwa eneo la Umoga na Jiji la Dodoma.
Wafanyabiashara hao pia wamedai kuwa licha ya agizo la serikali kupitia Waziri Mkuu la kumwaga kifusi katika eneo hilo jipya, bado utekelezaji wake haujakamilika.
“Tulielezwa kifusi kinachotakiwa ni magari 18, lakini hadi sasa ni kiasi kidogo tu kimewekwa,” amedai mmoja wa wafanyabiashara hao.
Mbali na hilo, wamedai kuwa eneo lao la awali lenye ukubwa wa mita za mraba 8,000 limepunguzwa, huku sehemu nyingine ikidaiwa kuuzwa bila maelezo ya kina.
Hata hivyo wamesema kuwa licha ya eneo hilo kutolewa na serikali, bado halina miundombinu ya maji, umeme pamoja na choo.
Akijibu malalamiko hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Nsubisi Kapura alisema ucheleweshaji unaoonekana unatokana na wafanyabiashara wenyewe kushindwa kufuata taratibu zilizowekwa.
Amesema Jiji tayari liliwaandikia barua ya mkataba kwa ajili ya matumizi ya eneo hilo, lakini wafanyabiashara hao wamekataa kuusaini.
Aidha ameeleza kuwa baadhi yao wanataka kuanza kutumia eneo hilo bila kulipia gharama zozote za awali, huku pia wakihitaji kuongezewa wafanyabiashara 50 ambao hawapo kwenye orodha rasmi.
“Sisi kama viongozi wa jiji tunawahitaji wakubaliane na utaratibu wa kukaa kwa mkataba. Eneo hili ni mali ya Serikali, hivyo kisheria hawawezi kulitumia bila mkataba. Hata Waziri Mkuu aliwahi kusisitiza umuhimu wa mikataba katika uendeshaji wa masoko,” amesema.









0 Comments