Na Samweli Mwanga, Maswa.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Maswa mkoani Simiyu kimemtunuku cheti cha pongezi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, kwa kutambua utendaji wake mzuri wa kazi.
Cheti hicho kilikabidhiwa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Maswa, Mwl Onesmo Makota, mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilayani humo. Makota alisema kuwa uamuzi wa kumtunuku Mtipa umetokana na juhudi na ufanisi aliouonesha tangu alipohamishiwa katika wilaya hiyo.
“Tumeshuhudia mabadiliko chanya katika utendaji wa halmashauri, na hii ni matokeo ya uongozi makini na uwajibikaji wake,” alisema Makota.
Akizungumza mara baada ya kupokea cheti hicho, Mtipa aliishukuru CCM wilaya ya Maswa kwa kutambua mchango wake, akiahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuwaletea maendeleo wananchi.
“Ninapokea heshima hii kwa unyenyekevu mkubwa. Ni motisha kwangu kuongeza juhudi katika kuwatumikia wananchi wa Maswa,” alisema Mtipa.
Katika hafla hiyo, viongozi wengine waliotunukiwa vyeti vya pongezi ni Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt Vicent Naano, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Variety Miza, Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, Dkt George Lugomela, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki.
CCM wilaya ya Maswa imesema itaendelea kutambua na kuthamini watendaji na viongozi wanaochangia maendeleo ya wananchi kupitia utendaji bora wa majukumu yao.
Mwisho.






0 Comments