Rais wa Kenya William Ruto ametoa wito wa ushirikiano wa kikanda na ushirikiano wa kiuchumi, akizitaka Kenya na Tanzania kuimarisha uhusiano wa uwekezaji na kuepuka tofauti zinazogawanya majirani hao wawili.
Akihutubia bunge la Tanzania mjini Dodoma siku ya Jumanne , Ruto amesema kwamba binafsi anaunga mkono juhudi za kuvutia uwekezaji Tanga, ikiwa ni pamoja na pendekezo la ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta, akisema kuwa mradi huo utanufaisha ukanda wa Afrika Mashariki.
"Binafsi, ninasaidia kuleta uwekezaji Tanga," alisema.
"Kama mngekuwa watu wazuri, mngekuwa mnasema asante kwetu Wakenya, tufanye kazi kama Afrika Mashariki.
Kenya iliwahi kumiliki kiwanda cha kusafisha mafuta cha Mombasa, ambacho awali kilijulikana kama Kenya Petroleum Refineries Ltd (KPRL) huko Changamwe, kabla ya kilisitisha shughuli zake za kusafisha mafuta ghafi mnamo Septemba 2013 kutokana na uzembe, gharama kubwa za uendeshaji na ufilisi wa kiufundi.
Baadaye kituo hicho kilichukuliwa na kumilikiwa na Kampuni ya Kenya Pipeline (KPC) ili kutumika kama ghala la bidhaa za petroli zilizosafishwa kutoka nje.
Lakini akizungumza mjini Dodoma, Rais Ruto alisisitiza kwamba maendeleo ya kiuchumi katika nchi moja hayapaswi kuangaliwa kwa kutengwa na majirani zake, akibainisha kuwa Kenya na Tanzania zina mustakabali mmoja.
"Kinachofaa kwa Tanzania ni kizuri kwa Kenya na kinyume chake. Naomba tuwe watu wamoja. Tusiruhusu mazungumzo ya jana yatutenganishe," alisema.
Ruto alisisitiza zaidi kuwa Kenya na Tanzania hazipaswi kuonana kama washindani au wapinzani, bali kama washirika katika maendeleo.
"Tuna hatima ya pamoja," alisema. "Nimeeleza kuwa Wakenya sio adui zenu na kinyume chake.
MWISHO.





0 Comments