KATIKA Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli – Bunju, Jimbo Katoliki la Bagamoyo, zoezi la upandaji miti limeendelea likiwa sehemu ya kampeni maalum ya mazingira inayoratibiwa na ANIELI Foundation kwa kushirikiana na viongozi wa Kanisa hilo pamoja na wadau wengine wa maendeleo.
ANIELI Foundation ni taasisi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na shughuli za kijamii katika sekta za afya, elimu na mazingira, ikiwa na lengo la kuboresha maisha ya Watanzania kupitia miradi endelevu ya maendeleo.
Kampeni hiyo inalenga kupanda zaidi ya miti 500 katika maeneo ya kijamii, ikiwemo maeneo ya kanisa, shule, makaburi, viwanja vya kijamii na kwenye makazi, kwa lengo la kuongeza uoto wa asili na kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Paroko wa Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli – Bunju, iliyopo wilayani Kinondoni Jijini Dar es salaam, Padre Dominic Somola, ameongoza shughuli hiyo kwa msisitizo kwamba utunzaji wa mazingira ni wajibu wa kiimani na kijamii.
Amesema kuwa kila mti unapopandwa, jamii inawekeza kwenye afya, hewa safi na ustawi wa vizazi vijavyo.
Mwenyekiti wa ANIELI Foundation, Gaudens Aniceth Mushi (Kanyaka), anaeleza kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya mpango mpana wa taasisi hiyo katika kuimarisha maisha ya jamii kupitia mazingira bora.
Ameongeza kuwa upandaji miti si tukio la mara moja bali ni utamaduni unaopaswa kujengwa katika kila kaya.
Katibu wa ANIELI Foundation,Wakili Wilhad Kitaly, amesema taasisi hiyo imeendelea kutoa elimu kwa watoto na vijana kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira ili kujenga kizazi chenye uelewa wa muda mrefu.
Katibu Msaidizi wa ANIELI Foundation, Octavian Kiwale, amesema kuwa mpango wa upandaji miti utaendelea kupanuka hadi maeneo ya vijijini ili kuhakikisha uoto wa asili unaimarika zaidi.
Kwa upande wa Brigedia Jenerali Mstaafu Adolf Muta, ambaye ni Katibu wa Umoja wa Wanaume Wakatoliki, UWAKA, Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli – Bunju, anasema jamii inapaswa kuona mazingira kama sehemu ya ibada na maisha ya kila siku.
Naye Nicolas James Buretta, Mwenyekiti Msaidizi wa Kamati Tendaji ya Parokia hiyo amesema ushirikiano kati ya taasisi za dini na mashirika ya kijamii ndio unaoweza kuleta matokeo chanya kwa jamii.
Kauli mbiu ya kampeni hiyo ni "Otesha Miti, Boresha Mazingira.”












0 Comments