Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio Daima
SERIKALI imewataka wadau wa ufugaji kushirikiana ili kufanya ufugaji wa kisasa, wenye tija na wa kibiashara.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ali, amesema uzalishaji katika sekta ya ufugaji kwa sasa bado si wa tija unaohitajika.
“Tunahitaji kuuza nyama nje ya nchi kufikia tani milioni 50 kutoka tani milioni 24 za sasa, nali kufikia huko ni lazima kufuga kisasa na kibiashara,” alisema Balozi Dkt. Bashiru Ali.
Akifungua mkutano wa Siku ya Nyanda za Malisho, Waziri alisema ufugaji wa kisasa unahusisha mifugo kupata lishe bora na kuwa na afya nzuri vinavyotokana na malisho bora.
Dkt. Bashiru alisema malisho bora ni lazima yaambatane na miundombinu muhimu ikiwemo nyasi, maji, pamoja na usimamizi na utunzaji mzuri.
“Ni muhimu kuanzishwa skimu za umwagiliaji, mashamba na vitalu vya mbegu za malisho pamoja na mashamba darasa ili kupata malisho bora,” alisema Waziri.
Alisema pia maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya malisho yanapaswa kusimamiwa kwa ushirikiano na wanufaika wa ardhi hiyo, wakiwemo wafugaji wenyewe.
Katika hotuba yake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena, alisema serikali inawashauri wadau wa ufugaji kuwekeza katika uzalishaji wa vyakula vya mifugo.
Alisema pia uzalishaji wa mbegu za malisho na vipando umeongezeka hadi tani 489.83 kutoka mashamba ya serikali na binafsi.
Katibu Mkuu huyo alisema serikali inaendelea kuwahamasisha wawekezaji na wafugaji kutumia mbegu hizo ili kuendeleza uwanda wa malisho, hasa wakati wa kiangazi.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)




0 Comments