Header Ads Widget

SERIKALI KUBORESHA MAZINGIRA YA UCHIMBAJI NA BIASHARA YA MADINI YA METALI NCHINI*



▪️  Waziri Mavunde asikiliza na kutatua changamoto za wadau wa madini ya metali

▪️ Aagiza kuanzishwa kwa Jukwaa la kudumu kati ya Serikali na wachimbaji na wafanyabiashara wa madini

▪️ Maabara ya kisasa ya madini inayojengwa Dodoma kutatua changamoto ya uchunguzi wa sampuli za madini

▪️Mfumo wa malipo ya mrabaha kuangaliwa upya

▪️ Wadau waahidi kushirikiana na Serikali kuongeza tija na mapato ya Taifa

📍Dodoma

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amewataka wadau wa madini ya metali (base metals) kujipanga kimkakati na kuifanya sekta hiyo kuwa kichocheo kipya cha ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini, akisisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa rasilimali, uwekezaji katika teknolojia za kisasa, uongezaji thamani, pamoja na kuzingatia misingi ya uwajibikaji na uwazi ni nguzo kuu za kuongeza tija, thamani na ushindani wa madini hayo katika soko la madini hayo. 

Amesema kuwa kupitia mbinu hizo, sekta ndogo ya madini ya metali ina uwezo mkubwa wa kufungua fursa za ajira, kuongeza mapato ya Taifa na kuimarisha mnyororo wa thamani wa viwanda, hivyo kuchangia kwa kiwango kikubwa katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi shindani na wa viwanda endelevu.

Amesema hayo leo Aprili 20, 2026 wakati akizungumza katika kikao na wadau wa Tanzania Base Metal Association (TBMA) kilichofanyika katika Ukumbi wa Tume ya Madini Jijini Dodoma, ambako amesema Serikali ina dhamira ya dhati ya kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji ili sekta hiyo iweze kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

“Mwelekeo wetu ni kuhakikisha sekta ndogo ya madini ya metali inakuwa na mchango mkubwa zaidi katika uchumi. Tutahakikisha changamoto zinazowakabili wadau zinapatiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu,” amesisitiza Mhe. Mavunde.

Mhe. Mavunde ametumia kikao hicho kusikiliza na kupokea changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wa madini ya metali, ikiwemo masuala ya miundombinu na masoko, huku akiagiza uanzishwaji wa Kituo cha Madini eneo la Mlongo-Kyerwa mahususi kwa ajili ya wachimbaji wa madini bati (tin) huku akiahidi kuzifanyia kazi kwa haraka ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji katika sekta hiyo.

Katika kuimarisha ubora wa huduma za kitaalamu za upimaji wa sampuli za madini, Waziri Mavunde amesema kuwa, Serikali inaendelea na ujenzi wa maabara ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli za madini katika eneo la Kizota, jijini Dodoma, mradi unaotarajiwa kuongeza ufanisi wa uchambuzi wa madini na kupunguza gharama kwa wachimbaji na wawekezaji.

Katika hatua ya kuongeza upatikanaji wa mitaji, Waziri Mavunde ameelekeza kuanzishwa kwa mfuko wa dhamana (Export credit guarantee scheme) utakaowezesha wachimbaji wadogo kupata mikopo yenye masharti nafuu, hatua inayotarajiwa kuongeza uzalishaji na ushindani katika soko la kimataifa.

Aidha, ameagiza Tume ya Madini kuanzisha jukwaa la kudumu kwa kushirikiana na wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini, litakalokuwa likikutana mara kwa mara kujadili changamoto na kupendekeza maboresho ya kisera na kiutendaji kwa lengo la kukuza sekta hiyo kwa ufanisi zaidi.

Pia, Mhe. Mavunde amesisitiza Serikali inaendelea kuboresha miundombinu katika maeneo yote yenye shughuli za madini, ikiwemo barabara na huduma za nishati, ili kuwezesha usafirishaji wa madini na kupunguza gharama za uzalishaji.

Mhe. Mavunde amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kukutana na wadau mara kwa mara ili kuimarisha ushirikiano, akibainisha kuwa mafanikio ya Sekta ya Madini yategemea mshikamano na uwazi kati ya Serikali na sekta binafsi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TBMA Godfrey Kente, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kushirikiana nao katika kutatua changamoto za sekta hiyo, akiahidi kuongeza uwekezaji na uzalishaji ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza mapato ya Taifa.



 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI