Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
SERIKALI imepanga kuanzisha ofisi maalum za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika maeneo ya vyama vya ushirika ili kulinda thamani na mali za wanachama dhidi ya vitendo vya ubadhirifu.
Akizungumza jijini Dodoma katika Mkutano wa Wadau wa Maendeleo ya Ushirika, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha uwajibikaji na kuongeza uadilifu katika usimamizi wa rasilimali za vyama vya ushirika.Amesema uwepo wa ofisi hizo utasaidia kufuatilia kwa karibu mienendo ya kifedha na utendaji wa viongozi wa ushirika, pamoja na kuchukua hatua za haraka pale vitendo vya rushwa au ubadhirifu vinapobainika.
“Tunataka kuhakikisha mali na fedha za wanachama zinalindwa ipasavyo kwa kuweka mifumo madhubuti ya usimamizi na udhibiti,” amesema Chongolo.
Ameongeza kuwa vyama vya ushirika vinazungusha fedha nyingi zenye thamani inayokadiriwa kufikia trilioni 6 hali inayohitaji uangalizi wa karibu na mifumo imara ya usimamizi ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa manufaa ya wanachama.
Aidha, amesema hatua hiyo itaenda sambamba na mapendekezo ya kuanzishwa kwa mifumo mingine ya udhibiti ikiwemo polisi maalum wa ushirika na ofisi za mashtaka zitakazoshughulikia kesi za ushirika kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, amesema kuwa mpango huo ni sehemu ya kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu” inayolenga kupunguza ubadhirifu, kuongeza uwazi na kuimarisha uaminifu ndani ya vyama vya ushirika.
Amebainisha kuwa kampeni hiyo itatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na itakuwa ikifanyiwa tathmini kila mwaka ili kupima mafanikio na kubaini changamoto.
Aidha, kampeni hiyo itajikita katika matumizi ya mifumo ya kidijitali, ukaguzi wa mara kwa mara, pamoja na kuanzishwa kwa mifumo ya kupokea taarifa kutoka kwa wadau na watoa taarifa (whistleblowers) ili kusaidia kudhibiti vitendo vya rushwa na ubadhirifu.
Pia, ameongeza kuwa kutakuwepo na maafisa uadilifu (integrity officers) ndani ya vyama vya ushirika watakaosaidia kusimamia nidhamu ya kifedha na kuhakikisha taratibu zinafuatwa ipasavyo.
Serikali inaamini kuwa kupitia hatua hizi, vyama vya ushirika vitaweza kuimarika zaidi, kuongeza ufanisi, na kuwanufaisha wanachama wake huku vikichangia ukuaji wa uchumi wa taifa.










0 Comments