WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeongeza kasi ya kuimarisha nidhamu na uwajibikaji ndani ya Jeshi la Uhifadhi, baada ya maafisa na askari 53 wa Kanda ya Kaskazini kupandishwa vyeo na kuaswa kuwa mfano wa kuigwa katika utumishi wa umma.
Akizungumza Aprili 2, 2026, wakati wa hafla ya uvishaji vyeo iliyofanyika wilayani Same, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia Utawala, SACC Erasto Luoga, aliyemwakilisha Kamishina wa Uhifadhi wa TFS, alisisitiza kuwa vyeo hivyo si tu ishara ya mafanikio binafsi bali ni dhamana nzito inayopaswa kuakisiwa kwa vitendo kupitia uadilifu, uwajibikaji na nidhamu ya hali ya juu.
“Cheo ni dhamana. Ni matokeo ya utendaji kazi uliotukuka, lakini pia ni mwanzo wa majukumu mapya yenye matarajio makubwa zaidi kutoka kwa taasisi na jamii,” alisema SACC Luoga, akiwataka waliopandishwa vyeo kuongeza juhudi katika kulinda rasilimali za misitu na kuimarisha taswira ya TFS.
Aliongeza kuwa maafisa hao wanapaswa kuzingatia kikamilifu maadili ya kazi na misingi ya utumishi wa umma, huku wakihakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi, ufanisi na uaminifu usiotiliwa shaka.
Kwa upande wake, Kamanda wa Kanda ya Kaskazini, SACC James Nshare, alimshukuru Kamishina wa Uhifadhi kwa kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi pamoja na upatikanaji wa vitendea kazi, akiahidi kuwa kanda hiyo itaongeza bidii ili kufikia malengo ya taasisi kwa ufanisi mkubwa.
“Kanda ya Kaskazini itaendelea kusimamia kwa vitendo maadili, nidhamu na utendaji wenye tija ili kuhakikisha tunalinda rasilimali za taifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema SACC Nshare.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa usalama na uhifadhi wilayani Same, akiwemo OCD, DSO na DAS, pamoja na wawakilishi kutoka taasisi za uhifadhi zikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, TAWA, TANAPA na Jeshi la Polisi.
Hatua hiyo inaakisi dhamira ya TFS ya kuendelea kujenga Jeshi la Uhifadhi lenye weledi, uadilifu na uwezo wa kukabiliana na changamoto za uhifadhi wa rasilimali za misitu nchini.


















0 Comments