Header Ads Widget

MAAFISA MAZINGIRA WAMETAKIWA KUSHIRIKIANA NA NEMC ILI KUAPATA MIONGOZO SAHIHI YA USIMAMIZI WA MAZINGIRA.


NA CHAUSIKU SAID, MATUKIO DAIMA MWANZA 


MWANZA, Maafisa mazingira Mkoani Mwanza wametakiwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ili kupata miongozo sahihi ya usimamizi wa mazingira, huku wananchi wakihimizwa kufuata na kusimamia utekelezaji wa Sheria Namba 191 ya mwaka 2004 iliyoboreshwa mwaka 2023, kwani wanao wajibu wa kutunza mazingira.


Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda na kueleza kuwa Mkoa wa mwanza unakumbwa na changamoto mbalimbali za kimazingira, ikiwemo uchafuzi wa Ziwa Victoria, ongezeko la takataka za plastiki, athari za uchimbaji wa madini, na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kibinadamu.


Mtanda, ameleza kuwa wananchi, na wadau wa serikali, na wadau mbalimbali kushirikiana katika kudhibiti uchafuzi wa mazingira, huku akisisitiza kuwa changamoto kubwa ya uchafuzi inahitaji hatua za pamoja kutoka kwa pande zote za kijamii, kiuchumi, na kisiasa.


"Uchafuzi wa mazingira si tu unaweza kuathiri mazingira, bali pia afya za wananchi na uchumi wa mkoa huu ni wakati wa kuchukua hatua za dharura kwa kushirikiana na wadau wote ili kuhakikisha kuwa tunalinda maliasili zetu kwa ajili ya vizazi vijavyo," alisema Mtanda.


Aidha ameleza kuwa Ziwa Victoria, ambalo ni chanzo kikuu cha uchumi wa Mkoa wa Mwanza limekuwa na uchafuzi mkubwa unaotokana na shughuli za kibinadamu. Uchafuzi huu unahusisha magugu maji, maji machafu yanayotiririka kutoka kwa majitaka na shughuli za kilimo, pamoja na athari za uvuvi na usafirishaji wa majini.


Mtanda alieleza kuwa serikali kwa kushirikiana na taasisi za mazingira, kama vile Bonde la Ziwa Victoria na NEMC, wanaendelea kuchukua hatua za kupunguza uchafuzi huo, lakini kuna haja ya kuongeza juhudi za elimu na usimamizi wa sheria za mazingira.


Pamoja na uchafuzi wa Ziwa Victoria, tatizo la takataka za plastiki limekuwa changamoto kubwa kwa mkoa wa Mwanza. Hata baada ya serikali kuanzisha sheria inayokataza matumizi ya mifuko ya plastiki, Mkoa umekutana na changamoto ya kuzagaa kwa mifuko ya plastiki katika maeneo ya wazi, mitaani, na kando ya Ziwa Victoria.


Mtanda alieleza kuwa licha ya kuwepo kwa sheria hii, bado kuna baadhi ya wafanyabiashara na wananchi wanaendelea kutumia mifuko ya plastiki, jambo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira. Alisema kuwa kuna haja ya kuongeza juhudi katika kutoa elimu kuhusu athari za plastiki na kuhakikisha kuwa sheria hii inatekelezwa kikamilifu.


“Serikali kupitia NEMC inafanya kazi kubwa katika kupambana na takataka za plastiki. Hata hivyo, kila mmoja wetu anawajibika katika kuhakikisha kuwa tunapunguza matumizi ya plastiki. Wafanyabiashara na wananchi wanapaswa kuzingatia sheria hii ili kulinda mazingira yetu,” alisema Mhe. Mtanda.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Usimamizi wa Sheria ya Mazingira kutoka NEMC, Bw. Elbarik Bajuta, alisisitiza kuwa NEMC inaendelea kushirikiana na viongozi wa Mkoa wa Mwanza katika kutoa elimu kwa wananchi na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria.



"Tumefanya vikao na viongozi wa Mkoa wa Mwanza na kujadili masuala ya uzingatiaji wa sheria za mazingira. Pamoja na kutoa elimu kwa wananchi, tunafanya ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha kuwa sheria za mazingira zinatekelezwa ipasavyo," alisema Bw. Bajuta.


Kwa upande mwingine, Bi. Sylvia Autophace, mtaalamu wa masuala ya kimazingira kutoka kampuni ya Nyanza Road Works Ltd, alieleza kuwa ni muhimu kwa wataalamu wa mazingira kutoa ushauri sahihi kwa wawekezaji ili kuhakikisha kuwa miradi ya madini inafanyika kwa kuzingatia mazingira.


"Wawekezaji lazima waelewe kuwa mazingira ni rasilimali muhimu. Tunapofanya kazi na wawekezaji, tunahitaji kuhakikisha kuwa wanatekeleza miradi yao kwa njia endelevu inayohakikisha usalama wa mazingira na afya za wananchi," alisema Bi. Autophace.


Mwanasheria kutoka Ziwa Steel and Wire Products Ltd, Philipo Sylivanus, ameeleza kuwa changamoto zinazozikumba sekta ya uwekezaji katika usajili wa miradi na usimamizi wa vibali vya mazingira.


Sylivanus alieleza kuwa wadau wengi wanapokuwa wanasajili miradi, mara nyingi wamekuwa wakiacha jukumu la usajili kwa wataalamu wa mazingira (environmental experts), lakini wao kama wenye miradi hawafuatilii maendeleo ya mchakato huo kwa karibu.


“Vikao kama hivi vinatusaidia hata sisi kama wawekezaji tunapaswa kuhakikisha kwamba tunafuatilia kwa karibu maendeleo ya miradi yetu Wakati mwingine tunaachia wataalamu wa mazingira wasajili miradi yetu, lakini kama wenye miradi, hatufuatilii kwa umakini kama mchakato unafanyika kama ilivyopangwa.


Mwisho 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI