Matukio Daima, Morogoro
Takribani kaya milioni 4.6 nchini zinategemea tasnia ya maziwa kwa kipato cha kila siku, hali inayoonesha umuhimu mkubwa wa sekta hiyo katika maisha ya wananchi na ustawi wa jamii.
Licha ya mchango huo, wadau wanasema bado kuna changamoto ya uelewa mdogo kwa baadhi ya wananchi kuhusu matumizi ya maziwa, hali inayosababisha kushuka kwa matumizi na kukwamisha ukuaji wa sekta hiyo.
Akizungumza mkoani Morogoro, Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), George Msalya, amesema maboresho ya uzalishaji na ukusanyaji wa maziwa ni muhimu katika kuongeza tija na kukuza sekta hiyo inayochangia asilimia 2 ya pato la taifa.
Kwa upande wake, mfanyakazi wa Bodi ya Maziwa Tanzania kituo cha Arusha, Chrisbel Swai, amesema kuna haja ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuondoa dhana potofu kuhusu matumizi ya maziwa na kuwahamasisha wananchi kutumia bidhaa hizo kwa wingi.
Naye Hamisi Athmani, muuzaji wa maziwa mkoani Morogoro, amesema mwamko wa matumizi ya maziwa umeanza kuongezeka kadri wananchi wanavyoendelea kupata elimu, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi hizo ili kuongeza kipato kwa wafanyabiashara na wazalishaji.
Wadau wa sekta hiyo wanaamini kuwa kuongeza uelewa kwa jamii kutachochea matumizi ya maziwa na kusaidia kukuza uchumi wa wananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)




0 Comments