Dodoma:
WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kutumia kalamu zao na kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuihamasisha jamii kujua namba zao za afya ili iweze kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kujenga taifa imara na lenye afya bora.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelezea miradi ya maendeleo inayofanywa na taasisi hiyo leo April 9,2026 katika ukumbi wa idara ya Habari Maelezo uliopo jijini Dodoma.
Dkt. Kisenge alisema JKCI inafanya kampeni ya “Jua Namba Zako” kuwataka wananchi kujua shinikizo la damu, kiwango cha sukari kwenye damu, urefu, uzito, mafuta mwilini, mapigo ya moyo, na utendaji kazi wa moyo lengo likiwa kupunguza idadi ya watu wanaopata magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.
“Kampeni zote zinazofanywa na JKCI ikiwemo hii ya jua namba zako na ile ya kuwafuata wananchi mahali walipo kuwafanyia uchunguzi wa afya zinatokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hususan katika kuboresha afya za wananchi na kurahisisha upatikanaji wa huduma bingwa bobezi za moyo”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema magonjwa ya moyo yanaendelea kuwa chanzo kikuu cha vifo duniani yakisababisha takribani vifo milioni 17.9 kila mwaka kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani, huku asilimia kubwa ya vifo hivyo ikitokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati ikiwemo Tanzania.
“Katika bara la Afrika ni nchi chache tu zimefanikiwa kuwa na hospitali maalum za matibabu ya moyo kutokana na gharama kubwa za uwekezaji zinazohitajika. Hata hivyo Tanzania imefanikiwa kuwa miongoni mwa nchi hizo huku JKCI ikitajwa kuwa kinara wa huduma za moyo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema JKCI kwa sasa inafanya upasuaji wa moyo kwa zaidi ya wagonjwa 3,000 wa moyo kwa njia ya tundu dogo kwa mwaka, ikiwa ni idadi kubwa ikilinganishwa na taasisi nyingine za ukanda wa Africa. Aidha taasisi hiyo inafanya upasuaji mkubwa wa moyo kwa zaidi ya wagonjwa wa moyo 800 kwa mwaka.
Mbali na upasuaji Dkt. Kisenge alisema JKCI imefanikiwa kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuanzisha matawi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Dar es Salaam, Arusha na Chato hatua inayosaidia kupunguza msongamano na kuongeza upatikanaji wa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wakati.
Katika kuimarisha huduma Dkt. Kisenge alisema taasisi hiyo imewekeza katika matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo mfumo wa ufuatiliaji wa wagonjwa kwa kutumia akili bandia (AI) pamoja na huduma za kuweka miadi mtandaoni hatua iliyopunguza muda wa kusubiri huduma hospitalini na kuongeza ufanisi.
“Tumeanzisha mchakato wa huduma za upandikizaji wa moyo nchini ambapo maandalizi yanaendelea ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wetu kwa kuwapeleka katika hospitali za kimataifa kwaajili ya mafunzo maalum”, alisema Dkt. Kisenge
Aidha Dkt. Kisenge alisema katika jitihada za kupanua huduma kimataifa JKCI imekuwa ikihudumia wagonjwa kutoka nchi mbalimbali ndani na nje ya Afrika hali inayochangia kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii wa matibabu ya moyo na kuongeza mchango katika uchumi wa taifa.
“Kwa mwaka 2025 pekee JKCI ilitoa huduma kwa zaidi ya wagonjwa 252,000 na kuendelea kutoa huduma za tiba mkoba katika mikoa 26 na zaidi ya wilaya 10 nchini ili kuwafikia wananchi wengi zaidi hususan walioko maeneo ya mbali na huduma bingwa bobezi za moyo.









0 Comments