Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio DaimaApp
JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro linaendelea kufanya uchunguzi wa ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha magari mawili kugongana uso kwa uso na kusababisha vifo vya watu watatu pamoja na majeruhi watano.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Andrew Kantimbo, alisema ajali hiyo ilitokea Aprili 21, 2026 majira ya asubuhi katika eneo la Kona S, kitongoji cha Kikoni, kijiji cha Lumango, kata ya Kidodi, tarafa ya Mikumi, wilaya ya Kipolisi Ruhemba mkoani Morogoro, katika barabara kuu ya Mikumi–Kilombero.
Alisema kuwa ajali hiyo ilihusisha gari aina ya lori (FAW) lenye namba za usajili T154 ECP/T229 EBY, lililokuwa likiendeshwa na Yasin Omary Nasiri (48), mkazi wa Dar es Salaam, likitokea Mikumi kuelekea Ruaha. Inadaiwa kuwa dereva huyo alijaribu kulipita gari la magurudumu matatu (Toyo) lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari, hali iliyosababisha kugongana uso kwa uso na basi aina ya Tata lenye namba T996 EPP la kampuni ya ZL Supper, lililokuwa likiendeshwa na Emanuel Benito kutoka Ifakara kuelekea Dodoma.
Kutokana na ajali hiyo, watu watatu walipoteza maisha papo hapo, akiwemo dereva wa lori hilo, Yasin Omary Nasiri (48), mkazi wa Dar es Salaam; Awadhi Ngwanda (60), fundi bomba, mkazi wa Mang’ula; pamoja na Zalaph Awadhi Ngwanda (20), mkazi wa Mang’ula.
Aidha, watu watano walijeruhiwa katika ajali hiyo, akiwemo mwanaume mmoja ambaye bado hajafahamika jina lake, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 40 hadi 45. Wengine ni Amani Iddi (60), mkulima mkazi wa Ifakara; Matha John (39), mfanyabiashara mkazi wa Dodoma; Pendo Kui (68), mkulima mkazi wa Singida; pamoja na Monica Lameck Mazuwameli (16), mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Iwemba, mkazi wa Lumango.
Majeruhi wote wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya St. Kizito iliyopo Mikumi.
Upelelezi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori aliyefanya jaribio la kupita bila tahadhari.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limetoa wito kwa madereva na watumiaji wote wa barabara kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha madhara makubwa.
Pia Kamanda Kantimbo ameonya kuwa hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya madereva wote wazembe.






0 Comments