Header Ads Widget

WANAWAKE VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA KILIMANJARO WAGUSA MIOYO YA WAFUNGWA KARANGA



Na Mwandishi Wetu, Moshi

Maafisa na askari wanawake kutoka vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama mkoani Kilimanjaro, leo Machi 6, 2026, wametoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa wafungwa na mahabusu wa Gereza Kuu Karanga lililopo Manispaa ya Moshi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kitakachofanyika Machi 8, 2026.

Wanawake hao kutoka taasisi mbalimbali wakiwemo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Magereza, Idara ya Uhamiaji, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Jeshi la Akiba, waliungana kwa pamoja kufika gerezani hapo na kukabidhi msaada kwa wafungwa na mahabusu waliopo.

Misaada iliyotolewa ni pamoja na sukari kilo 100, sabuni, taulo za kike, majora ya vitambaa kwa ajili ya kushonea sare za wafungwa wa kike, mafuta ya kupaka pamoja na dawa za meno, ikiwa ni sehemu ya mchango wao wa kijamii kwa kundi hilo maalum.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mhifadhi wa TFS, Zayana Mrisho, alisema hatua hiyo inaonesha namna wanawake wanavyoweza kutumia maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani si tu kwa sherehe bali pia kwa vitendo vya huruma na kujali makundi yenye uhitaji katika jamii.

Alisema wanawake wana jukumu kubwa katika kuhamasisha mshikamano wa kijamii na kuleta matumaini kwa watu wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo wale waliopo katika mazingira ya kifungo.




Akizungumza mara baada ya kupokea misaada hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Gereza, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza (SSP) Godbless Moshi, aliwashukuru wanawake hao kwa moyo wao wa kujitoa na kuonesha mshikamano kwa wafungwa na mahabusu wa gereza hilo.

Alisema msaada huo umeleta faraja kubwa kwa walengwa na kuonesha mchango muhimu wa wanawake katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii, huku akisisitiza kuwa vitendo vya namna hiyo vinaongeza ari na matumaini kwa wafungwa wanaotumikia adhabu zao.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani hufanyika kila mwaka Machi 8, yakilenga kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii, kuhimiza usawa wa kijinsia na kuhamasisha uwezeshaji wa wanawake katika sekta mbalimbali.

Katika picha ni baadhi ya matukio ya wanawake kutoka vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na TFS walipowatembelea wafungwa na mahabusu katika Gereza Kuu Karanga, Moshi, na kukabidhi misaada hiyo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI