Header Ads Widget

KAMATI YA SIASA CCM TABORA YARIDHISHWA NA UJENZI WA KITUO CHA MBEGU TFS KALIUA



Na Mwandishi Wetu, Kaliua

Kaliua, Machi 6, 2026 – Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora imeonyesha kuridhishwa na kiwango cha utekelezaji na ubora wa ujenzi wa Kituo cha Mbegu cha Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kilichopo wilayani Kaliua, ujenzi unaofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO).

Ziara ya Kamati ya Siasa iliyofanyika jana iliongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Mhe. Said Nkumba (MNEC), akiongozana na Ndg. Abdan Nassoro, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Ndg. Wilson Tambaku, Katibu wa CCM Mkoa (MNEC), pamoja na viongozi wengine wa chama na serikali. Wengine waliokuwapo ni pamoja na Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu, Mhe. Masanja Lufungija, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Mhe. Dkt. Gerald Mongella, na viongozi wengine wa wilaya.

Mratibu wa Mradi ngazi ya Kanda, Mhifadhi Linda Shio, alisema ujenzi wa kituo hicho unatekelezwa chini ya Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo katika Maeneo ya Nyanda Kame (DSL-IP), unaolenga kupunguza uharibifu wa ardhi na kupotea kwa bioanuai. Mradi huu unashirikisha sekta za kilimo, mifugo, maji na nishati safi, na unatekelezwa katika nchi 11 huku Tanzania ikiwa na miradi katika mikoa ya Tabora na Katavi.

Wilayani Kaliua, mradi unajumuisha pia ujenzi wa mabanda ya kufungia nyuki na kituo cha kuchakata asali, hatua inayolenga kuongeza thamani ya mazao ya misitu na kuboresha kipato cha wananchi.




Kituo cha Mbegu cha TFS Kaliua kimegharimu Shilingi milioni 585, ukiwekwa mkandarasi wake SADITECK Investment Limited wa Dar es Salaam. Kaimu Mhifadhi Misitu Wilaya ya Kaliua, SCO Sadock Gobanya, alisema kituo hicho kitakuwa na jukumu la kukusanya, kuhifadhi na kusambaza mbegu bora za miti ya asili ya jamii ya miombo kama mitundu, mininga, mikurungu, mibanga, mikora na miyombo.

Gobanya alibainisha kuwa kituo hicho pia kitakuwa kitovu cha tafiti na elimu kuhusu uhifadhi wa miti ya asili, huku kikitengeneza ajira kupitia ukusanyaji na uuzaji wa mbegu. Uwepo wa kituo huo utasaidia kurejesha uoto wa miombo ulioathiriwa na shughuli za kibinadamu.

Eng. Haji Shambani Matikulu, Msimamizi wa Ujenzi, alisema majengo yanayojengwa yamefikia asilimia 98, ikiwa ni pamoja na jengo la kupokea na kuandaa mbegu, jengo la utawala lenye maabara ya kisasa na vyumba vya kuhifadhi mbegu kwa teknolojia ya kisasa. Changamoto iliyopo ni kuchelewa kuunganishiwa huduma ya umeme kutoka TANESCO, hali inayochelewesha kuonesha matumizi ya mitambo na mfumo wa kamera za ulinzi (CCTV).

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Ndg. Said Nkumba, alisema Kamati ya Siasa imeridhishwa na ubora wa ujenzi na matumizi sahihi ya fedha. Aliongeza kuwa uwepo wa maabara ya kisasa utasaidia katika tafiti za upatikanaji wa aina bora za miti ya asili, huku akimpongeza mkandarasi na uongozi wa Wilaya kwa ushirikiano katika kusimamia miradi ya maendeleo.

“Jitihada hizi zitasaidia ukusanyaji na uhifadhi wa mbegu za miti ya asili na hivyo kuwezesha kurejesha uoto wa miombo unaoathiriwa na shughuli za kibinadamu,” alisema Nkumba.

Kamati pia ilisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kituo kinawanufaisha wananchi wa Kaliua kwa ajira na elimu ya ukusanyaji na uhifadhi wa mbegu za miti ya miombo. Kituo hicho kinatarajiwa kurahisisha upatikanaji wa mbegu bora za miti ya asili kwa mikoa ya ukanda wa magharibi na kusaidia juhudi za serikali kurejesha uoto wa asili.

Mwisho wa ziara, Mwenyekiti wa CCM Mkoa aliomba Kamati ya Siasa itembelee tena kituo hicho mara baada ya kuanza rasmi kazi, ili kujifunza zaidi kuhusu teknolojia ya kisasa ya uhifadhi wa mbegu za miti ya asili.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI