Header Ads Widget

WANANCHI KARAGWE WAIOMBA SERIKALI KUWAUNGANISHIA UMEME

 

Na Anold Deogratias Matukioa Daima Media Kagera

Wananchi wanaoishi katikati mwa mitaa miwili ya Bomani na mtaa wa Miti katika mji mdogo wa Kayanga wilyani Karagwe mkoani Kagera wameomba serikali kupitia shirika la umeme  nchini TANESCO mkoa wa Kagera kuwaunganishia huduma ya umeme ili kuwaondolea adha wanayoipata ya maeneo yao kutokuwa na huduma hiyo.

Wakizungumza na vyombo vya habari wananchi hao akiwemo Saulo Samweli mkazi wa Mtaa Miti Kayanga amesema kuwa kukosekana kwa huduma hiyo katika mitaa yao inapelekea kushindwa kukuza uchumi wao kupitia shughuli za kiuchumi.

“kukosekana kwa umeme tunashindwa kufanya shughuli muhumi kama kuanzisha viwanda vidogo vidogo ambavyo vingetusaidia kukuza uchumi wetu lakini pia tunakaa kwenye giza tunaiomba serikali na sisi itukumbuke laini kubwa zinapita katika mitaa yetu ila sisi hatuna umeme”

Naye Joyness Raulian amesema kuwa wamekuwa wakipewa ahadi za kuunganishiwa umeme kwa muda mrefu lakini bado hawajapata huduma hiyo hali inayowarudisha nyuma kimaendeleo.

“tumekuwa tunaomba umeme kwa TANESCO lakini bado hatujapata umeme umeambiwa tusubili laini ndogo, hapa zinapita laini kubwa zienda kijiji Jirani lakini kwetu hatuna sisi tumesahaulika hatuna huduma nyingi hata na barabara”

Mwenyekiti wa mtaa wa Bomani Gidioni Machage amesema kuwa eneo hilo limesahaulika kwa muda mrefu katika huduma muhimu  za kijamii kama umeme na barabara na kuziomba mamlaka husika kuwapelekea huduma hizo ili kuwaondolea adha wananchi.

“maeneo hay oni kweli yamekuwa na changamoto ikiwemo umeme na barabara, me naomba serikali na mamlaka husika kama TANESCO na TARURA kufikisha huduma hizo ili kuwarahisishia wananchi kufanya shughuli zao kwa urahisi”

Kwa upande wake Kaimu Meneja TANESCO Kagera, MhandisiThobias Mutalemwa amesema kuwa mkandarasi kwa ajili ya kuwaunganishia umeme wananchi wa mitaa hiyo tiyari ameishapatikana na kwa sasa yupo kwenye hatua za kukusanya vifaa vya kuunganisha umeme katika maeneo hayo na kuwataka wananchi kuwa wavumilivu.

“mkandarasi tayari ameishapatikana na kwa sasa yupo katika hatua ya kukusanya vifaa na mara baada ya kukusanya vifaa ataanza kutekeleza mradi wa M300 ambao unahusisha maeneo hayo yaliyopo katika mji wa Kayanga wilayani Karagwe”

Itakumbukwa shirika la umeme TANESCO mkoa wa Kagera lina mpango wa kuziunganishia umeme kaya laki tatu na elfu kumi na tano kwa muda wa miaka 5 ijayo hivyo kumaliza adha ya ukosefu wa huduma ya umeme kwa maeneo yote mkoa wa Kagera.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI