Na. John I. Bera, Iringa
Vituo vya Askari wa Wanyamapori vinavyojengwa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika maeneo mbalimbambali yanayopakana na Hitadhi za Taifa hapa nchini vimekuwa vya msaada mkubwa kwa wananchi wanapopata changamoto ya wananyamapori wakali na waharibifu.
Akizungumza katika Kijiji cha Mbolimboli, kilichopo Iringa Vijijini, katika eneo linalopakana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha Afisa Wanyamapori Mkuu, wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Julius Kimaro, amesema kituo hicho ni miongoni mwa vituo muhimu vinavyotumika kutoa mwitikio wa haraka pindi wanyamapori wanapoingia katika makazi ya wananchi na kusababisha madhara.
“Maeneo haya yamekuwa yakikumbwa na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu, hususan tembo ambao wamekuwa wakivamia na kuharibu mali za wananchi na kuhatarisha usalama wao. Uwepo wa kituo hiki umepunguza kwa kiasi kikubwa matukio hayo.”
Amesema kuwa eneo hilo hukumbwa na wingi wa migongano baina ya binadamu na wanyamapori hivyo kuhitaji kuwepo kwa kituo cha askari wanyamapori.
“ Wanyamapori wamekuwa wakifika katika maeneo haya na kusababisha migongano kutokea mara kwa mara, hivyo uwepo wa kituo hiki ni muhimu na kimesaidia kupunguza migongano hiyo. Wananchi sasa wanaishi kwa amani na mali zao ziko salama.”
Kwa upande wake, Askari Mhifadhi Daraja la II, Christopher Rocky amesema tangu kukamilika kwa kituo hicho, askari wamekuwa wakifika kwa wakati katika maeneo yanayoripotiwa kuvamiwa na wanyamapori wakali na waharibifu.
“Kabla ya ujenzi wa kituo hiki, askari walikuwa wakitoka makao makuu Iringa na wengine Migoli, hivyo kuchukua muda mrefu kufika eneo la tukio. Lakini sasa askari wanakaa hapa kituoni, tunafika haraka na kudhibiti wanyamapori kabla hawajasababisha madhara.”
Naye Askari wa Wanyamapori wa Vijiji (VGS), Ally Muhehe, amesema ushirikiano kati ya askari na wananchi umeimarika tangu kuanzishwa kwa kituo hicho.
Muhehe amesema wananchi wanafurahia juhudi za serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kujengwa kwa kituo hicho ambacho kimesaidia kuongezeka kwa usalama wa wananchi na mali zao.








0 Comments