Header Ads Widget

UJENZI DARAJA LA MAWE MATONGO KUCHOCHEA UZALISHAJI MALI TARIME VIJIJINI.


📌Mradi wa Cerc waibua matumaini uchimbaji madini,mifugo na biashara

Tarime - Mara

Imeelezwa kuwa kukamilika kwa ujenzi wa daraja la mawe la Matongo lenye urefu wa mita 41 linalojengwa katika barabara ya Matongo - Nyarwana katika mto Pigite litachochea shughuli za uzalishaji mali ikiwemo uchimbaji madini katika mgodi wa Nyamongo uliopo katika Kata ya Matongo Halmashauri ya Wilaya Tarime Vijijini.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Tarime Mhandisi Charles Marwa wakati wa ziara maalum ya kutembelea miradi inayotekelezwa kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato wilayani humo. 

Daraja hilo linalojengwa kupitia Mfuko wa Dharura unaofadhaliwa na Benki ya Dunia (CERC) linaunganisha Kata za Matongo na Kibasuka ambazo ni maarufu kwa shughuli za kilimo, ufugaji na uchimbaji wa madini katika Halmashauri hiyo.

Mhandisi Marwa amesema kabla ya ujenzi huo wananchi walikuwa wanavuka kwa kutumia kidaraja kilichojengwa juu ya mti wa Mkuyu kwa malipo ya shilingi 1000 kwa mtu mzima na shilingi 500 kwa watoto wadogo. 

"Uvukaji wa pale haukuwa mzuri kwa sababu ulikuwa ni hatarishi kutokana ujenzi wa kidaraja hicho kutumia miti ambayo pia ni hatarishi". amesema Mhandisi Marwa.

Ameendelea kufafanua kuwa kutokana na hali hiyo Serikali imepeleka fedha na sasa wanajenga daraja ambalo limefikia takriban asilimia 70 na kuongeza kuwa barabara za maingilio Km 2.6 zimeshatengenezwa kwa kiwango cha changarawe na kwa sasa wanajiandaa kumwaga zege la deki Ili daraja lianze kutoa huduma.

Akielezea umuhimu wa daraja hilo kiuchumi na kijamii Mhandisi Marwa amesema eneo la Matongo kuna mnada ambao hufanyika mara kwa mara lakini pia kata ya Matongo, eneo la Nyamongo ndiko shughuli za uzalishaji mali hususani uchimbaji wa madini katika mgodi wa Nyamongo zinafanyika hivyo kiunganishi kilikuwa kinakosekana, amefafanua Mhandisi Marwa.

"Daraja hili ni ukombozi kwa sababu ukiangalia siku za mnada ule mto ukiwa umefurika ng'ombe zilikuwa zinavushwa kwa kuogelea pamoja na watu hali ambayo ilikuwa ni hatari lakini Sasa ng'ombe zitapita, watu watapita na huduma itakuwa ni bora sana kwa watu wetu na litachochea uzalishaji mali pamoja na kuboresha maisha ya mtu mmoja mmoja" amebainisha.

Naye, Baraka Mahanga Kidebe Mkazi wa Kijiji cha Nyarwana amesema wao kama wananchi wa kata ya Kibasuka wanashukuru kwa kazi inayofanyika ya ujenzi wa daraja hilo pamoja na barabara kwani kabla ya ujenzi wa daraja hilo walikuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya uvukaji katika eneo hilo. 

Kwa upande wake Nchagwa Mesenda Magige Mkazi wa Kata ya Matongo   amesema kabla ya ujenzi wa daraja hilo walikuwa wanapata shida kwenda kupata mahitaji huko Nyamongo na siku za mnada unaofanyika Matongo. 

Amesema kwa ujio wa barabara na daraja hilo wanaona sasa wanaenda kupata haki yao wananchi wa Kata ya Matongo.



 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI