Header Ads Widget

SERIKALI YATOA BILIONI SITA KUKABILI POLIO KWA WATOTO MILIONI SITA KWA MIKOA SABA


Mwanza

Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi bilioni Sita kwa ajili ya chanjo ya polio ya matone itakayotolewa kwa watoto milioni Sita chini ya miaka 10 kwa mikoa Saba ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita, Tabora, Singida pamoja na Mara. 

Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin Shigela amesema hayo leo Machi 24, 2025 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza akimuwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa kwenye uzinduzi wa kampeni ya chanjo ya polio ya matone mkoani Mwanza. 

"Tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu huu na kutoa fedha hizo, zaidi ya miaka 30 Tanzania haina ugonjwa huu lakini zipo nchi jirani bado ugonjwa huu upo, chanjo yetu hii inaandaa watoto wetu ili waweze kuimarisha kinga zao na kukabiliana na ugonjwa huu wa polio," amesema Mhe. Shigela 

Aidha, Mhe. Shigela amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa timu zitakazozunguka katika mikoa hiyo ili watoto chini ya miaka 10 wapate chanjo ya polio kwa awamu hii ya kwanza itakayotolewa kwa siku Nne kuanzia tarehe 24 - 27 Machi, 2026. 

"Niwaombe sana waheshimiwa Viongozi tujipange kuhakikisha tunahamasisha wazazi/walezi kuwapela watoto kupata chanjo katika maeneo yanayotolewa ili kumkinga mtoto asipate ugonjwa wa polio na sio kusubiri siku ya mwisho ndio idadi kubwa inajitokeza," amesema Mhe. Shigela 

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema katika mikoa yote Saba zipo timu elfu kumi na nne (14,000) ambazo zitatoa huduma hizi za chanjo ya polio ya matone, 

"Ili tuweze kuwafikia watoto wengi chanjo hizi zitatolewa kwenye vituo vyetu vya tiba (zahanati, vituo vya afya, hospitali), maeneo mbalimbali ya mukusanyiko (kanisani, msikitini, sokoni, stand ya mabasi na kwenye magulio)," amesema Dkt. Magembe 

Dkt. Magembe ametumia fursa hiyo kuwatoa hofu wananchi kuwa chanjo hiyo ni salama, haina madhara yeyote kimwili wala kiakili kwa watoto wote wanaopata chanjo hiyo ya polio na chanjo nyingine na kubainisha kuwa chanjo ni kinga. 

"Kwa nini tunatoa chanjo hii?, ni kwa sababu mtoto yeyote anaweza kupata magonjwa haya na kueneza kutoka kwa mtoto mmoja kwenda kwa mtoto mwengine hivyo kuweza kuwakinga maambukizi haya yasiwepo, chanjo ni afua inayofanya kazi vizuri sana," amesema Dkt. Magembe





 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI