Na Matukio Daima Habari, Mbeya
WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Mbeya umeeleza kuwa serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa njia ya mchepuo katika eneo la Iwambi–Mbalizi, hatua ambayo inalenga kupunguza msongamano na ajali, sambamba na kurahisisha shughuli za usafirishaji kwa wananchi.
Imeelezwa kuwa barabara hiyo ya mchepuo tayari imeanza kutumika kwa kiwango fulani, huku changamoto iliyokuwa ikichelewesha kukamilika kwa ujenzi huo ikiwa ni uwepo wa nguzo za umeme ambazo zinaunganishwa na mkoa wa Songwe pamoja na kiwanda cha saruji kilichopo eneo hilo.
Akizungumza Machi 3, 2026 mara baada ya kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mbeya, Meneja wa TANROADS mkoa wa Mbeya, Suleiman Bishanga, amesema kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) liko hatua za mwisho kuondoa nguzo hizo ili kuruhusu mkandarasi kuendelea na kazi bila vikwazo.
“Jitihada zinaendelea. Meneja wa TANESCO yuko kwenye hatua za mwisho kuhakikisha nguzo zinaondolewa. Mkandarasi ameridhia kuendelea na kazi, na muda si mrefu barabara hii itakamilika. Wananchi watanufaika na ajali zitapungua. Ikumbukwe kuwa Mheshimiwa Rais Samia aliagiza changamoto hizi zitatuliwe,” amesema Bishanga.
Ujenzi wa Barabara ya Mbalizi–Shigamba Waendelea
Kuhusu maendeleo ya barabara ya Mbalizi kuelekea Shigamba, Bishanga alisema kuwa upembuzi yakinifu na usanifu makini wa barabara hiyo unaendelea sambamba na maeneo ya Kimo na Kafafa, huku upande wa Songwe barabara hiyo ikiwa ni kiunganishi muhimu kuelekea Itumba na Isongole.
“Wananchi tunawahakikishia kuwa kipande cha kwanza cha lami kimetengwa na serikali. Mkandarasi tayari amepatikana na atajenga kilomita 10, kuanzia Mbalizi hadi Shigamba,” amefafanua.
Ujenzi wa Barabara ya Isonje–Kikondo kuimarishwa
Katika hatua nyingine, Bishanga amesema serikali imeagiza maeneo yote korofi katika barabara ya Isonje–Kikondo, inayounganisha mkoa wa Mbeya na Njombe, yawekwe zege ili kurahisisha safari za wakulima na wananchi wanaosafirisha mazao kutoka Makete kwenda Mbeya.
Mwisho.






0 Comments