Header Ads Widget

SERIKALI IMEANDAA MKAKATI WA KUKABILIANA NA UJANGILI WA WANYAMAPORI NCHINI.


NA,Jusline Marco:Arusha.

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Ashatu Kijaji amesema kupungua kwa wanyamapori kutokana na uvamizi wa mapori kwa shughuli za kibinadamu, ujangili na biashara haramu ya nyara, ongezeko la mimea vamizi pamoja na mabadiliko ya tabia ya nchi ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta ya utalii nchini.

Waziri Kijaji ameyabainisha hayo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori Duniani ambayo kitaifa yamefanyika Macho 3,2026 jijini Arusha, ambapo pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuhimiza uhifadhi, kukuza utalii na kusimamia utunzaji wa mazingira.

Aidha amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau imeandaa mikakati mbalimbali kukabiliana na changamoto hizo, ikiwemo kupambana na ujangili wa nyara, kuokoa na kulinda shoroba za wanyamapori, kutekeleza mpango mkakati wa kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu kwa kununua vifaa vya kisasa vinavyotumia teknolojia ili kunusuru maisha ya Watanzania, pamoja na kuimarisha doria kupitia taasisi za maliasili na utalii.

Amesema maadhimisho hayo ni kumbukizi ya mkataba wa kimataifa wa wanyama na mimea iliyo katika hatari ya kutoweka, na kusisitiza kuwa Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi muhimu duniani kwa kuwa na wanyamapori wengi, ikiongoza kwa idadi ya wanyama kama chui na simba, huku ikiwa ya tatu duniani kwa kuwa na tembo wengi.

Ameongeza kuwa sekta ya utalii inachangia asilimia 25 ya mapato ya fedha za kigeni na asilimia 17.1 ya Pato la Taifa, pamoja na kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya milioni 1.6.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Nkoba Mabula, amesema kuwa ofisi yake itasimamia kikamilifu maelekezo yote yaliyotolewa ili kuhakikisha uhifadhi unaendelea kuwa neema kwa watanzania na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amesema taasisi zote zilizoshiriki katika maadhimisho hayo zina ushirikiano mkubwa na Serikali na wananchi, na zimekuwa chachu ya kujifunza masuala ya uhifadhi.

Shughuli za maadhimisho hayo zilifanyika kwa namna mbalimbali ikiwemo makongamano, huku kipaumbele kikubwa kikiwa ni upandaji miti katika shule za jijini Arusha, ikiwemo Shule ya Sekondari Mringa.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI