Mojtaba Khamenei, mwana wa Ayatollah Ali Khamenei wa Iran ambaye aliuawa katika mashambulizi ya Marekani na Israeli, amechaguliwa kuwa mrithi wake.
Tofauti na baba yake, mtu huyo mwenye umri wa miaka 56 kwa kiasi kikubwa si mtu aliyekuwa akijitokeza hadharani. Hajawahi kushikilia wadhifa wa serikali, wala kutoa hotuba za hadharani au mahojiano, na ni idadi ndogo tu ya picha na video zake ambazo zimewahi kuchapishwa.
Lakini kwa miaka mingi kumekuwa na uvumi kwamba alikuwa na ushawishi mkubwa nyuma ya pazia nchini Iran.
Nyenzo za kidiplomasia za Marekani, ambazo zilichapishwa na WikiLeaks mwishoni mwa miaka ya 2000, zilimtaja kama "nguvu nyuma ya pazia" ambaye alichukuliwa sana kama mtu "mwenye uwezo na nguvu" ndani ya utawala, kulingana na shirika la habari la AP.
Hata hivyo uteuzi wake bado unaweza kuwa na utata. Jamhuri ya Kiislamu ilianzishwa mwaka wa 1979 baada ya utawala wa kifalme kupinduliwa, na itikadi yake inategemea kanuni kwamba kiongozi mkuu anapaswa kuchaguliwa kwa sababu ya msimamo wake wa kidini na uongozi uliothibitishwa, si kwa kurithi.
Wakati wa utawala wake, Ali Khamenei alizungumzia kwa ujumla tu kuhusu uongozi wa baadaye wa Jamhuri ya Kiislamu.
Mjumbe mmoja wa Baraza la Wataalamu la Iran, chombo cha makasisi kinachomchagua kiongozi mkuu - alisema miaka miwili iliyopita kwamba Ali Khamenei alipinga wazo la mwanawe kuwa mgombea wa uongozi wa baadaye. Lakini hajawahi kuzungumzia hadharani kuhusu hilo.
MOJTABA KHAMENEI NI NANI?
Mojtaba Khamenei alizaliwa tarehe 8 Septemba 1969 katika mji wa Mashhad ulioko kaskazini mashariki mwa Iran. Yeye ni mtoto wa pili kati ya watoto sita wa Ali Khamenei. Alipata elimu yake ya sekondari katika Shule ya Alavi huko Tehran.
Akiwa na umri wa miaka 17, Mojtaba alihudumu jeshini kwa vipindi vifupi wakati wa vita vya Iran–Iraq, kulingana na vyombo vya habari vya Iran.
Vita hivyo vya miaka minane vilivyojaa umwagaji damu vilifanya serikali ya Iran kuwa na mashaka makubwa zaidi dhidi ya Marekani na nchi za Magharibi, ambazo zilikuwa zinaunga mkono Iraq.
Mwaka 1999, Mojtaba alikwenda Qom, mji mtakatifu unaochukuliwa kuwa kituo muhimu cha theolojia ya Shia, ili kuendelea na masomo yake ya kidini. Inasemekana kuwa hakuvua mavazi ya kidini hadi wakati huo, na haijulikani vizuri kwa nini aliamua kujiunga na seminari akiwa na umri wa miaka 30, kwani kwa kawaida watu huanza masomo hayo wakiwa wadogo zaidi.
Hadi sasa, Mojtaba bado ni kiongozi wa dini wa ngazi ya kati . Hali hii inaweza kuwa kikwazo kwake iwapo atajaribu kupanda hadi kuwa kiongozi mkuu wa Iran.
Katika siku za hivi karibuni, baadhi ya vyombo vya habari na maafisa walio karibu na vituo vya mamlaka nchini Iran wameanza kumtaja Mojtaba Khamenei kama "Ayatollah", cheo cha juu cha kidini.
Mabadiliko haya yanaonekana kwa baadhi ya wachunguzi kama jaribio la kuinua hadhi yake ya kidini na kumwonesha kama kiongozi anayeweza kuaminika.
Katika mfumo wa masomo ya seminari, kushika cheo cha "Ayatollah" na kufundisha madarasa ya juu ya kidini huchukuliwa kuwa ishara ya kiwango cha juu cha elimu na ujuzi wa mtu. Hali hii pia huonekana kama moja ya masharti muhimu katika mchakato wa kumchagua kiongozi wa baadaye.
Hata hivyo, tayari kuna mfano wa tukio kama hilo hapo awali. Ali Khamenei alipandishwa haraka cheo na kuitwa "Ayatollah" baada ya kuwa Kiongozi Mkuu wa pili wa Iran mwaka 1989.
TUHUMA ZA KUINGILIA SIASA.
Jina la Mojtaba Khamenei lilianza kujulikana sana kwa umma wakati wa uchaguzi wa urais wa mwaka 2005, ambao ulisababisha ushindi wa Mahmoud Ahmadinejad, mwanasiasa mwenye msimamo mkali wa kihafidhina na mtetezi wa sera za watu wa kawaida.
Katika barua ya wazi kwa Ali Khamenei, mgombea wa mageuzi Mehdi Karroubi alimshutumu Mojtaba kwa kuingilia mchakato wa upigaji kura kupitia baadhi ya wanachama wa Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC) na wanamgambo wa Basij, ambao walidaiwa kugawa fedha kwa makundi ya kidini ili kumsaidia Ahmadinejad kushinda.
Miaka minne baadaye, Mojtaba alikabiliwa tena na tuhuma hizo hizo. Kuchaguliwa tena kwa Ahmadinejad kulisababisha maandamano makubwa kote nchini. Baadhi ya waandamanaji walipaza sauti wakipinga wazo kwamba Mojtaba ataweza kumrithi baba yake kama Kiongozi Mkuu wa Iran.
Mostafa Tajzadeh, ambaye wakati huo alikuwa naibu waziri wa mambo ya ndani, alielezea matokeo ya uchaguzi huo kama "mapinduzi ya uchaguzi". Baadaye alifungwa gerezani kwa miaka saba, jambo ambalo alisema lilitokana na "matakwa ya moja kwa moja ya Mojtaba Khamenei."
Wagombea wawili wa mageuzi, Mir-Hossein Mousavi na Mehdi Karroubi, waliwekwa kifungo cha nyumbani baada ya uchaguzi wa mwaka 2009. Mwezi Februari 2012, Mojtaba alikutana na Mousavi na kumshawishi aache maandamano yake, kulingana na vyanzo vya Iran vilivyonukuliwa na BBC News Persian.
Sasa watu wengi wanatarajia Mojtaba ataendelea na sera kali za baba yake, Ali Khamenei.
Baadhi pia wanaamini kwamba mtu ambaye amepoteza baba yake, mama yake na mke wake katika mashambulizi la Marekani na Israel, huenda asiwe tayari kukubali shinikizo la nchi za Magharibi.
Hata hivyo, anakabiliwa na kazi ngumu sana ya kuhakikisha uendelevu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, pamoja na kuwashawishi wananchi kwamba yeye ndiye mtu sahihi wa kuiongoza nchi kutoka katika uharibifu wa kisiasa na kiuchumi.
Rekodi yake ya uongozi bado haijajaribiwa kwa kiwango kikubwa, na mtazamo kwamba jamhuri hiyo inageuka kuwa mfumo wa kurithishana madaraka ya kifamilia unaweza kuongeza zaidi kutokuridhika kwa wananchi.





0 Comments