Header Ads Widget

MICHE 1,000 YAPANDWA LINDI KUADHIMISHA SIKU YA MISITU DUNIANI



DC Mwanziva aongoza kampeni; wananchi wahimizwa kulinda misitu kwa uchumi endelevu


LINDI: 

Wananchi wa Mkoa wa Lindi wameungana na viongozi wa Serikali katika kuadhimisha Siku ya Misitu Duniani kwa kupanda miche 1,000 ya miti katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Lindi, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuhimiza uhifadhi wa misitu na upandaji miti.

Zoezi hilo liliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe. Victoria Mwanziva, kwa kushirikiana na Balozi wa Mazingira Michael Msechu pamoja na wahifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutoka Makao Makuu.

Upandaji huo wa miti ulifanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi Sokoine iliyopo Mitwero pamoja na Shule ya Msingi Mchinga I iliyopo katika Jimbo la Mchinga, ambapo viongozi hao waliwataka wananchi kuendelea kupanda miti na kuitunza ili kulinda mazingira na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, mhe. Mwanziva alisema misitu ni rasilimali muhimu inayochangia ustawi wa uchumi, afya ya mazingira na maisha ya wananchi, hivyo akawahimiza wakazi wa Lindi kushiriki kikamilifu katika kampeni ya upandaji miti inayoendelea mkoani humo.

“Tunapaswa kutambua kuwa misitu ni uhai wa taifa letu. Hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kupanda miti na kuitunza ili kizazi cha sasa na kijacho kiendelee kunufaika na rasilimali hii muhimu,” alisema.





Kwa upande wake, Balozi wa Mazingira Michael Msechu alisisitiza kuwa kampeni ya upandaji miti inalenga kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa misitu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kukuza uchumi wa wananchi kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za misitu.

Kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Dk. Zainabu Bungwa, Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali za Misitu na Nyuki, alisema misitu ni msingi wa uchumi endelevu wa taifa kwa kuwa ina faida za moja kwa moja kwa wananchi pamoja na huduma muhimu za kiikolojia.

Alieleza kuwa uwepo wa misitu unachangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa mvua, hewa safi, maendeleo ya kilimo, nishati inayotokana na maji pamoja na shughuli za umwagiliaji.

“Misitu ni uchumi. Mbali na faida za moja kwa moja, kuna huduma nyingi za kiikolojia zinazotegemea uwepo wake. Mvua, hewa safi, kilimo, nishati ya maji na umwagiliaji vyote vinategemea sana misitu,” alisema.

Aliongeza kuwa TFS iko tayari kuendelea kutoa elimu, utaalam na miche ya miti ili kuhakikisha Mkoa wa Lindi unaendelea kuwa wa kijani na kuchangia lengo la taifa la kuongeza uoto wa asili nchini.

Aidha, ilibainishwa kuwa miche yote iliyopandwa pamoja na utaalam wa upandaji ilitolewa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kama sehemu ya juhudi za Serikali za kuhamasisha uhifadhi wa misitu na mazingira.

Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani mwaka huu yanafanyika kitaifa Mkoani Lindi yakibebwa na kaulimbiu isemayo: “Misitu ni Uchumi Endelevu, Tuihifadhi kwa Maendeleo ya Taifa.”

Wakati maadhimisho hayo yakiendelea, halmashauri mbalimbali za wilaya mkoani humo zimeendelea kuhamasisha wananchi kupanda miti katika maeneo ya taasisi za umma, shule na makazi yao, pamoja na kushiriki katika maonesho yanayoambatana na maadhimisho hayo.








Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI