Header Ads Widget

MAKAMU WA RAIS AONGOZA MAADHIMISHO YA KILELE CHA WIKI YA MAJI 2026*




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ametoa wito kwa Mamlaka zinazohusika pamoja na Watanzania kwa ujumla kuweka kipaumbele katika utunzaji na ulinzi wa vya vyanzo vya maji ili kuweza kurithisha kizazi kijacho nchi inayofaa kuishi.
 
Makamu wa Rais ametoa wito huo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Maji kwa Mwaka 2026 na Siku ya Maji Duniani iliyofanyika katika Viwanja vya Mkwawa mkoani Morogoro leo tarehe 22 Machi 2026. Amesema ni lazima kuangalia sana umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji kwa kufanya uwekezaji wa kimkakati ambao unaangalia kuvitunza na kuongeza vyanzo vya maji.
 
Halikadhalika, Makamu wa Rais ametoa rai kwa Wizara na Taasisi zote za Umma nchini kujenga mtandao wa ushirikiano katika kuzikabili kuzitatua na kurekebisha changamoto za maji ili dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na Taifa lilioondokana na changamoto za maji safi na salama iweze kufanikiwa.
 
Pia amesema, ni vema kwa Mamlaka za Maji nchini kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kukuza sekta ya maji. Ameipongeza Mamlaka ya Maji Tanga kwa kutumia mfumo wa Hati fungani katika kugharamia miradi ya maji inayotekelezwa mkoani humo. Makamu wa Rais amesema kila mtanzania anapaswa kuona wajibu wa utunzaji wa mazingira.
 
Vilevile, Makamu wa Rais amesema, Sekta binafsi ni mdau muhimu katika kufanikisha miradi ya maji kwa maendeleo ya sekta hiyo. Ametoa wito kwa wadau wote wa sekta ya maji kutambua kwamba maji ni muhimu na hitaji la kila mwanadamu hivyo ni vema kuendelea kushirikiana.
 
Makamu wa Rais, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha mpango wa Gridi ya Taifa ya Maji unafanikiwa kikamilifu kwani kufanikiwa kwake ndio kuondokana na tatizo la maji nchini. Amewasihi Wizara ya Maji kuhakikisha wanafanikisha ufungaji wa mita katika maeneo ya matumizi ya maji ili kuepusha upotevu wa maji lakini pia kufanya watu wanaotumia maji kuwajibika.
 
Vilevile, Makamu wa Rais amesema Dira ya Maendeleo 2050 imelenga kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii, ambapo matarajio ni kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kipato cha kati ngazi ya juu. Wakati idadi ya watu nchini ikitarajiwa kuongezeka hadi kufikia takriban watu milioni 118, inatarajiwa pia kuwa zaidi ya nusu yao watakuwa wanaishi maeneo ya mijini. Ongezeko hilo la watu linahitaji kujipanga ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa chakula, fursa za ajira na huduma za kijamii kama afya na elimu na maji.
 
Moja ya malengo makuu ya Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2002, Toleo la 2025 ni kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi, hususan wanaoishi vijijini. Katika utekelezaji wa Sera hii na Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, miradi mbalimbali ya maji nchini imetekelezwa na kuwezesha kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi, ambapo kwa sasa vijijini huduma hiyo imefikia wastani wa 85.2%, na mjini wastani wa 92.5%. Jumla ya Vijiji 10,758 vimefikiwa na huduma ya maji, vikisalia Vijiji 1,575 ambavyo Wizara ya Maji imezindua kampeni maalum ya kuhakikisha inafikisha huduma hiyo.
 
Kwa upande wake, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha vema Wizara ya Maji kutekeleza miradi kwa ufanisi. Ameongeza kwamba, Wizara hiyo haitokuwa kikwazo katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
 
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amezindua Mfumo wa Utabiri wa Kiasi cha Maji kwenye mito nchini Tanzania. Uzinduzi huo umefanyika katika la Bwawa la Mindu Mjini Morogoro. Mfumo huo ni moja ya jitihada za Wizara ya Maji kuhakikishia inaondoa changamoto za Sekta kwa kuwezesha upatikanani wa taarifa sahihi za kiwango cha Maji katika mito yote nchini.
 
Pamoja na uzinduzi huo, Makamu wa Rais amepanda miti rafiki wa maji kwenye chanzo hicho ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani na kilele cha Wiki ya Maji Tanzania.
 
Maadhimisho hayo yana kaulimbiu isemayo “Maji na Usawa wa Kijinsia” (Water and Gender) yikilenga kutafakari kwa kina uhusiano uliopo kati ya upatikanaji wa maji safi na usawa wa kijinsia katika jamii. Ripoti ya Umoja wa Afrika kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Maji (mwaka 2023) inaonesha kuwa Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara inapoteza 5% ya Pato lake la Taifa kwa mwaka (takriban Dola za Marekani Bilioni 170) kutokana na ukosefu wa maji, matumizi ya maji yasiyo salama na ukosefu wa huduma bora za usafi wa mazingira.
 
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
22 Machi 2026
Morogoro.





 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI