Na. Edmund Salaho/ SERENGETI.
Kufuatia mabadiliko ya Tabia Nchi yaliyopelekea Mvua kubwa kuharibu Miundombinu ikiwemo Vivuko na Madaraja katika Hifadhi ya Taifa Serengeti Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajia kujenga madaraja matano katika maeneo korofi ndani ya hifadhi hiyo.
Akizungumza leo Machi 6, 2026 baada ya kukagua athari za mafuriko katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara - TANAPA, Massana Mwishawa alisema kuwa mbali na madaraja hayo makubwa pia kutajengwa madaraja mengine matano madogo katika maeneo yaliyoathiriwa na mvua hizo.
Aliongeza kuwa ujenzi wa madaraja hayo utakuwa suluhisho la kudumu la changamoto hiyo, kuboresha Mawasiliano ya Barabara na kuongeza Usalama kwa watalii na watumiaji wengine wa barabara. Aidha, pia waongoza watalii wamekumbushwa kuendelea kuchukua hatua za tahadhari hasa katika maeneo korofi na kufuata maelekezo wanayopewa na uongozi.
Kamishna Mwishawa ameongeza kuwa kwa miaka ya hivi karibuni hifadhi hiyo haijapata mvua kubwa kama zilizonyesha msimu huu na kuwa hadi sasa hakuna majeruhi wala vifo vilivyotokana na mafuriko hayo.
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi - Ismail Omar, alisema kuwa Hifadhi imewekeza nguvu kubwa katika maeneo matatu korofi ambapo kwa sasa hatua zinazoendelea kuchukuliwa ni pamoja na uokoaji kwa wanaokwama ambapo katika kila eneo kuna vikosi vya uokoji wakiwa na zana mbalimbali ikiwemo greda na trekta.
Kamishna Ismail, aliongeza kuwa mbali na kuwepo vikosi vya uokoaji, wanatumia ndege ambayo inabaini maeneo ambayo magari yamekwama na kuwatumia GPS wanatuma vikosi vya uokoaji kwenda kusaidia magari yaliyokwama.
Serikali ya Awamu ya Sita inakwenda kujenga madaraja katika eneo la Viboko vya Nabi, Mokasi, kwa Bona, Mto Banagi na kwa Lower wa Rangi.











0 Comments