Header Ads Widget

KISWAHILI CHATAMBA DUNIANI, WADAU WAKUTANA ARUSHA KULIJADILI

 


Na Pamela Mollel,Arusha


Kiswahili kinaendelea kung’ara kimataifa, kikijidhihirisha kama moja ya lugha zenye ushawishi mkubwa katika mawasiliano ya kidigitali na utandawazi.

Kwa kulitambua hilo, mkutano mkubwa wa kimataifa unaolenga kukuza na kuimarisha matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili umeanza rasmi Machi 24 jijini Arusha, ukikusanya wadau mbalimbali kujadili mustakabali wa lugha hiyo katika uwanja wa kimataifa.

Kongamano hilo la siku nne, litakalohitimishwa Machi 27, limewakutanisha washiriki kutoka nchi zaidi ya 38 wakiwemo wanahabari, wataalamu wa lugha, wabunifu wa maudhui ya kidigitali pamoja na watunga sera, kwa lengo la kuimarisha nafasi ya Kiswahili katika mawasiliano ya kimataifa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, alisema vyombo vya habari vina jukumu kubwa katika kukuza na kueneza Kiswahili ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Alisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya Kiswahili fasaha, akieleza kuwa hatua hiyo si tu inalinda lugha bali pia inaifanya kuwa chombo madhubuti cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.



Aidha, aliwahimiza vijana kutumia fursa zinazotokana na teknolojia ya kidigitali kwa kuunda maudhui bunifu yatakayochangia kueneza Kiswahili katika majukwaa ya kisasa duniani.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Sanaa na Utamaduni, Paul Makonda, alisema hatua ya UNESCO kuitambua Kiswahili kimataifa ni mafanikio makubwa kwa Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla.

Aliongeza kuwa utambuzi huo unafungua milango kwa taasisi za kimataifa kuanza kutumia Kiswahili katika mikutano na majadiliano rasmi, hali itakayoongeza hadhi na ushawishi wa lugha hiyo duniani.

Katika kongamano hilo, washiriki wanatarajiwa kujadili mada mbalimbali zikiwemo matumizi ya Kiswahili katika teknolojia, nafasi ya vyombo vya habari katika kukuza lugha hiyo, pamoja na fursa za ajira zinazotokana na ukuaji wa Kiswahili katika uchumi wa kidigitali.

Kwa ujumla, kongamano hilo linatajwa kuwa hatua muhimu katika safari ya kuiimarisha Kiswahili kama lugha ya kimataifa, huku likifungua milango ya fursa mpya za kiuchumi na kijamii kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla.





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI