Header Ads Widget

COCA-COLA YATOA BILIONI 5 KULINDA VYANZO VYA MAJI WAMI-RUVU



Matukio Daima, Morogoro 

KAMPUNI ya Coca-Cola kwa kushirikiana na IUCN na Serikali kupitia Bodi ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu, imezindua mradi wa zaidi ya Shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kulinda vyanzo vya maji katika kidakio cha Ngerengere mkoani Morogoro.

Mradi huo unaojulikana kama NBS4WATER unalenga kurejesha mazingira, kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji na kuboresha maisha ya wananchi wanaozunguka bonde hilo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo mjini Morogoro, Meneja Mkuu wa Coca-Cola Kwanza, David Chait alisema uwekezaji huo unalenga kuongeza upatikanaji wa maji salama kwa jamii ikiwemo wakazi wa Dar es Salaam.

Alisema Bonde la Wami-Ruvu ni muhimu kwa shughuli za kiuchumi na kijamii hivyo kuna haja ya kulinda vyanzo vyake.

Kwa upande wake, Meneja wa mradi kutoka IUCN, Doyi Mazenzele alisema zaidi ya wakulima 2,000 watanufaika kwa kufundishwa kilimo kinachokabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Aliongeza kuwa mradi utarejesha zaidi ya hekari 3,000 za ardhi na lita milioni 548 za maji.

Akizindua mradi huo kwaniaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Maji, Rosemary Rwegubisa alisema Serikali imepiga marufuku shughuli zote za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka vyanzo vya maji.

Alisema hatua mbadala zimewekwa ikiwemo upandaji miti, ufugaji nyuki na uchimbaji visima.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Bonde hilo, Juvenalis Tarimo alisema wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu kulinda rasilimali hizo huku zaidi ya watu 2,000 wakitarajiwa kunufaika.

Kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa Coca-Cola Afrika Mashariki na Kati, Alfred Olajide, mradi huo ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na changamoto ya uhaba wa maji duniani.

Uzinduzi huo umekwenda sambamba na upandaji miti kando kando ya Bwawa la Mindu Mjini Morogoro.






















Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI