Header Ads Widget

BUWASA,YAPANDA MITI KULINDA VYANZO VYA MAJI BUKOBA



NA MATUKIOA DAIMA NEWS


BUKOBA: 

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) imepanda jumla ya miti 1,000 katika mabwawa ya kutibu majitaka yaliyopo Kata ya Nyanga, Manispaa ya Bukoba, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Kaimu Mkurugenzi wa BUWASA, Mhandisi Lucas Selebeya, amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha uhifadhi wa mazingira hususani katika maeneo ya vyanzo vya maji ili kuhakikisha vinadumu kwa muda mrefu.

Amesema mamlaka hiyo imeona umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Wiki ya Maji kwa kufanya shughuli za vitendo, ikiwemo upandaji miti katika maeneo mbalimbali yenye vyanzo vya maji ili kuepuka uharibifu unaoweza kusababishwa na ukame.

Aidha, Mhandisi Selebeya ametoa wito kwa wananchi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji kujiepusha na shughuli zinazoweza kusababisha uchafuzi wa mazingira, akisisitiza kuwa ushirikiano wa jamii ni muhimu katika kulinda rasilimali hizo muhimu.

Ameongeza kuwa zoezi hilo linaendelea pia katika maeneo ya Muleba, Karagwe na Mutukula, ambapo BUWASA inatarajia kupanda zaidi ya miti 2,000 katika vyanzo mbalimbali vya maji.

Sambamba na hilo, mamlaka hiyo imetangaza ofa maalum kwa wateja waliokatishiwa huduma ya maji, ambapo watakaolipa nusu ya deni lao watarejeshewa huduma bila faini, huku salio lililobaki likilipwa kwa awamu. Ofa hiyo imeanza Machi 19, 2026 na itahitimishwa Machi 31, 2026, ikiwa na kaulimbiu ya mwaka huu isemayo, “Maji na Jinsia.”




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI