Na Lilian Kasenene, Morogoro-Matukio DaimaApp
MVUA zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini na kusababisha mafutiko yakiwemo ya wilaya ya Kilosa Morogoro zimesababisha athari ya uharibifu wa miundombinu, makazi ya watu kujaa maji, pamoja na kifo kimoja cha mama mwenye umri wa miaka 70 eneo la Kidete Stesheni alipokuwa kwenye jitihada za kuvuka Mto Mkondoa.
Mkuu wa wilaya ya Kilosa , Shaka Hamdu Shaka alisema hayo juzi mjini Kilosa kuwa mvua kubwa zilizonyesha Machi 9, mwaka huu zilileta athari maeneo ya Miyombo , Mhenda na Mkata Stesheni zilizopo wilayani humo.
Shaka alisema kwa haraka na tathimini iliyofanyika kuna baadhi ya makazi ya watu yameathirika kwa kiasi kikubwa ambapo eneo la Miyombo zaidi ya nyumba 100 zimeathirika kwa kuungiliwa na maji ya mafuriko ya mvua.
Shaka alisema kwa upande Miyombo kwa sasa mawasiliano yamefunguka hadi kufika eneo la Muhenda jambo kunahitajika ukarabati mkubwa wa barabara kutoka Kilosa- Muhenda kwa vile athari yake ni kubwa.
Pia alisema mafuriko hayo aliathiri eneo la Mkata Stesheni ambapo kwa siku ya juzi barabara ilifunga kabisa ingawa kwa sasa imeanza kupitika kwa tofauti na siku ya kwanza .
“ Kwa siku ya mafuriko hayo njia ilikuwa haipitiki ilikuwa lazima uzunmguke hadi Dumila – Mvomero , Morogoro na ndipo uende Mikumi “ alisema Shaka.
“ Kwa sasa tumekuwa na hofu ya m to Mkondoa kwa sababu maji ni mengi na endapo kina cha maji kikiongezeka kidogo kuna hatari ya maji kwenda kwenye makazi ya wananchi “ alisema Shaka
Mkuu wa wilaya alisema kutokana ana hali hiyo, Taasisi zinazohusika zitaweza kufika eneo la mto mkondoa ili kuona namna ya kuchukua jitihaza za haraka na za dharua.
Wakati huo huo, Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Adam Malima aliyetembelea eneo Barabara Mikumi – Ifakara baada ya Daraja namba nne lililopo eneo la Mikumi kukatika usiku Machi 9, 2026 na kusababisha adha kwa wananchi na huduma za usafiri.
Malima, akiwa katika eneo hilo aliwataka wananchi na watumiaji wa barabara hiyo kuwa na subira wakati Serikali ikiendelea kuchukua hatua za kurejesha mawasiliano hayo.
Malima aliwataka wataalaamu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) mkoa wa Morogoro kufanya kazi usiku na mchana ili kurejesha mawasiliano ya eneo hilo kwa haraka.
Malima alimwagiza Meneja wa TANROADS wa Mkoa huo kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi wake katika daraja hilo lililokatika.
“ Kwa sasa jitihada zinazofanywa na serikali ni kuimarisha kwa haraka eneo mojawapo ili kurahisisha wananchi kupita na ninawasii wenye magari makubwa kuwa na subira hadi hapo wataalamu watakapojiridhisha kutengemaa kwa Daraja hili” alisema Malima.
Mkuu wa mkoa huyo pia waliwaagiza wahansidisi wa Wakala huo kuwa na utaratibu wa kukagua madaraja mara kwa mara ili kuyafatia ukarabati na kunusuru maisha ya watu na mali zao.
Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa huo , Mhandisi Patrick Rambika, alisema athari hizo zilitokea usiku wa kuamkia Machi 9, 2026 na kuharibu madaraja hayo kukatika na kuleta athari ya usafiri na usafirishaji kwa maeneo ya Mikumi- Ifakara na kusitishwa kwa muda.
Nao baadhi ya wananchi na watumiaji wa barabara hiyo wameiomba Serikali kusaidia matengenezo ya barabara hiyo kukamilika mapema, kwa kuwa ni kiungo muhimu cha usafiri na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali ndani nan je ya Mkoa wa Morogoro.
Mwisho.











0 Comments