Wananchi wa Mkoa wa Kagera wameendelea kunufaika na Kliniki Tembezi ya Macho inayoendeshwa na Madaktari Bingwa wa Macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba kwa kushirikiana na Shirika la KCCO kwa ufadhili wa Australia Aid na The Fred Hollows Foundation.
Kupitia kliniki hiyo, wananchi wa Wilaya ya Muleba wamepata huduma za uchunguzi, matibabu, Miwani, Dawa na Ushauri Nasaha katika Kituo cha Afya Kamachumu huku wananchi wa Wilaya ya Missenyi wakinufaika na huduma hizo katika Zahanati ya Mutukula.
Huduma hizi zimekuwa mkombozi kwa wakazi wa maeneo ya pembezoni ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma za kibingwa za macho.
Sambamba na hilo, Kliniki Tembezi imewafikia wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaosoma katika Shule ya Msingi Kagondo B iliyopo Wilaya ya Muleba pamoja na Shule ya Msingi Bunazi iliyopo Wilaya ya Missenyi.
Wanafunzi hao wamepata huduma za uchunguzi wa macho, matibabu, dawa pamoja na ushauri nasaha bure hatua inayochangia kuboresha afya zao na maendeleo ya masomo.
Akizungumza na Madaktari hao Mkuu wa Shule ya Msingi Bunazi, Edwine Kahabuka alitoa shukrani kwa Madaktari Bingwa wa Macho, uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba pamoja na shirika la KCCO na wafadhili wao kwa kuendelea kuona umuhimu wa kuwafikia wanafunzi wenye mahitaji maalumu huku akisisitiza kuwa, huduma hizo zimeongeza uwezo wa uoni kwa wanafunzi hao na kusaidia kupiga hatua kimasomo ikilinganishwa na kipindi cha awali kabla ya kupatiwa huduma.
Kliniki tembezi inaendelea katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera, ambapo siku ya Ijumaa tarehe 13 Machi 2026 itafanyika katika Kituo cha Afya Rwamishenyi pamoja na Shule ya Msingi Mugeza Mseto iliyopo Manispaa ya Bukoba.
Aidha, kuanzia tarehe 23 hadi 27 Machi 2026, kambi hiyo itafanyika katika Kituo cha Afya Nkwenda kilichopo Wilaya ya Kyerwa.
Huduma zinazotolewa kupitia kliniki tembezi ni pamoja na uchunguzi na matibabu ya macho, utoaji wa miwani, dawa, huduma ya upasuaji kwa wananchi wanaogundulika kuwa na ugonjwa wa mtoto wa jicho pamoja na ushauri nasaha.















0 Comments