- Uzalishaji wa asali waruka mara tatu kwa miaka mitatu
Manyoni — Mkurugenzi wa Idara ya Misitu Zanzibar, Said Juma Ali, ameipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani Manyoni kwa kuimarisha usimamizi wa shughuli za ufugaji nyuki, hatua iliyochochea ongezeko kubwa la uzalishaji wa asali na nta pamoja na kuinua biashara ya mazao hayo kwa jamii.
Pongezi hizo amezitoa Februari 12, 2026 baada ya kupokea wasilisho la hali ya uzalishaji wa asali na nta kwa kipindi cha miaka mitatu (2022/2023–2024/2025) lililotolewa na Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Nyuki Manyoni, Igunda John, ikiwa ni sehemu ya ziara ya mafunzo ya wataalamu kutoka Zanzibar.
Akiwasilisha takwimu hizo, Igunda John, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Nyuki Manyoni, alisema uzalishaji wa asali umeongezeka kutoka kilo 4,992.6 mwaka 2022/2023 hadi kilo 14,665.7 mwaka 2024/2025, huku uzalishaji wa nta ukipanda kutoka kilo 159.8 hadi kilo 489 katika kipindi hicho — ongezeko linalokaribia mara tatu ndani ya miaka mitatu.
Alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na maboresho ya usimamizi wa mnyororo wa thamani kuanzia shambani, uvunaji, uhifadhi hadi hatua ya uchakataji, pamoja na kuimarika kwa mafunzo kwa wafugaji wa nyuki wilayani humo.
Akizungumza baada ya wasilisho hilo, Said alisema mafanikio hayo yanadhihirisha umuhimu wa elimu kwa jamii na usimamizi madhubuti wa rasilimali za nyuki.
“Ni dhahiri TFS Manyoni mmefanya kazi kubwa ya kuelimisha jamii kuhusu faida za kufuata kanuni bora za ufugaji nyuki. Hapo awali wengi hawakutambua thamani ya mazao ya nyuki, lakini sasa mwitikio ni mkubwa na wananchi wameanza kunufaika kiuchumi,” alisema.
Hata hivyo, aliwataka wataalamu kuendelea kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu, hususan kuhusu namna ya kutambua ubora wa asali na mazao mengine ya nyuki ili kulinda afya za watumiaji na kukuza soko la bidhaa halali.
Katika siku ya pili ya ziara yao, wataalamu kutoka Idara ya Misitu Zanzibar walitembelea Hifadhi ya Nyuki Aghondi na kujionea mifumo ya kisasa ya ufugaji, kabla ya kupata mafunzo ya uchakataji katika Kiwanda cha TFS Manyoni kinachoongeza thamani ya mazao hayo.
Ziara hiyo ya siku tano inalenga kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na TFS Bara katika kukuza sekta ya nyuki kama chanzo cha ajira, mapato na nyenzo muhimu katika uhifadhi wa misitu na bioanuai.











0 Comments