Na. Matukio Daima Media App, Zanzibar.
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), limewataka Wasanii kutumia majukwaa yao kukuza haki za watoto, kupinga mila na mitazamo potofu inayodhuru, na kuhamasisha mabadiliko chanya katika jamii
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Februaryi 5,2026 Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania, Elke Wisch, amesema UNICEF inawaomba wasanii hasa wanaoshiriki tamasha la Sauti za Busara 2026, kutumia majukwaa yao kukuza haki za watoto, kupinga mila na mitazamo potofu inayodhuru, na kuhamasisha mabadiliko chanya katika jamii.
Amesema muziki na maeneo mengine ya ubunifu yamekuwa na mchango mkubwa katika kuwaunganisha watu na kuchochea mabadiliko chanya. Wasanii wana uwezo wa kipekee kufikia hadhira pana, hususan katika matamasha kama Sauti za Busara, ambako watu hutoka maeneo mbalimbali kushiriki uzoefu wa pamoja.
“Kaulimbiu ya tamasha inatukumbusha kuwa kila mtoto huzaliwa na uwezo, kipaji na mwanga ndani yake. Hata hivyo, ili mwanga huo uangaze kikamilifu, watoto wanapaswa kukua wakiwa salama, wakilindwa na kuungwa mkono sio tu na familia, jamii zao, bali na sisi sote tukishirikiana," amesema Elke.
Na kuongeza; “UNICEF, kwa kushirikiana na Serikali na wadau wetu, hufanya kazi kila siku kuimarisha mifumo ambayo watoto wanategemea. Lazima tukomeshe ukatili dhidi ya watoto na tuwahakikishe wasichana na wavulana wanaendelea kuwa shuleni.”
Ili juhudi hizi ziwe na maana ya kweli, ni lazima tukabiliane na vikwazo vinavyozima uwezo wa watoto. Kuwafikia watu popote walipo, iwe ni katika jamii au kwenye matukio kama Sauti za Busara kunasaidia kuunda fursa za kuanzisha mazungumzo.” amesema Elke Wisch, Mwakilishi wa UNICEF.
![]() |
| Nabiha Kassim, Mwakilishi wa Vijana wa UNICEF |
Kwa upande, Nabiha Kassim, Mwakilishi wa Vijana wa UNICEF amesema mtoto hawezi kung’aa ikiwa anakumbana na ukatili katika mazingira yoyote, ikiwa anaishi kwa hofu, unyanyapaliwa au maumivu ya kimya na changamoto za afya ya akili
Nae Journey Ramadhani ambaye ni Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara ameendelea kuukumbusha umma kuwa tamasha hilo la msimu wa 23 linafanyikia viwanja vya Mnazi Moja February 5-8,2026.
“Kuanzia msanii mkuu wa tamasha Salif Keita kutoka Mali, hadi sauti zinazoongoza na zinazoibukia kutoka Tanzania, Afrika Kusini, Rwanda, Kenya, Uganda, Algeria, Nigeria na kwingineko, programu hii inawakutanisha vizazi na mitindo mbalimbali ya muziki.
“Zaidi ya majukwaa ya maonesho, tamasha linaendelea kuwekeza kwa wasanii kupitia majukwaa ya mitandao kama Movers and Shakers, yakitoa nafasi ya ushirikiano, kujifunza, na ukuaji wa muda mrefu ndani ya tasnia ya muziki barani Afrika.” amesema
Tamasha hilo ambalo linafanyika Unguja, Zanzibar, mwaka huu linaenda na kaulimbiu isemayo 'Let Them Shine' 'Waache Wang'are'. Huku likisisitiza wasanii kutumia vipaji vyao kuwa sauti ya haki kwa watoto.













0 Comments